Na Penina Malundo,TimesMajira.Online
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewahadharisha wakandarasi na wataalamu wa maji kutochelewesha miradi ya maji kwa kisingizio cha ukosekanaji wa mabomba ya kusafirishia maji ambayo kwa sasa yanazalishwa kwa wingi nchini.
Pia amesema hatamvumilia mkandarasi au mtaalamu yeyote wa maji, atakayechelewesha miradi hiyo kwa kisingizio cha kuagiza mabomba hayo nje ya nchi wakati ndani ya nchi, yanapatikana atahakikisha anapangiwa shughuli nyingine ya kufanya.
Ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam kwenye ziara ya kutembelea viwanda vinavyozalisha mabomba ya maji, ili kujiridhisha uwezo wa uzalishaji endapo unatosheleza mahitaji ya ndani, jambo litakaloondoa visingizio vya ucheleweshwaji wa miradi kwa wakandarasi waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi mbalimbali kwa kuwa, mabomba yanayotumika kusambaza maji yanapatikana hapa hapa nchini.
Waziri Aweso amesema, miradi iliyopo hadi sasa ni takribani 631 ya maeneo ya mijini na vijijini.
Amesema kutokana na kujionea kwa macho wingi wa uzalishaji wa mabomba ya maji katika viwanda hivyo, hakuna sababu wakandarasi hao, kusema miradi ya maji inacheleweshwa sababu ya miradi hiyo kuagizwa nje ya nchi.
Waziri Aweso amesema kwa sasa, hakuna haja ya kuagiza nje ya nchi mabomba hayo kwani yanapatikana nchini hivyo ni lazma kuunge mkono kwa vitendo jitihada za Rais Dkt. John Magufuli za kuviendeleza viwanda vya ndani.
“Lazma tuunge mkono kwa vitendo viwanda vya ndani hawa ni wenzetu, sisi hatutakuwa na sababu ya kuwa kikwazo tutatoa ushirikiano mkubwa, tujipange kuhakikisha mwaka 2025 dhamira ya kumtua mwanamama ndoo kichwani, inafanikiwa na hali ya upatikanaji wa maji asimilia 85 ya vijijini na asilimia 95 ya mijini yanapatikana,” amesema na kuongeza:
“Tumekuja kwenye ziara kwa sababu maji hayana mbadala wala porojo, hususan katika maeneo ya vijijini ambako kumekuwa na changamoto kubwa ya maji sasa kilio cha Rais Magufuli na wananchi ni upatikanaji wa maji,” amesema.
Amesema Rais Magufuli, anasisitiza uwekwaji wa mazingira rafiki na sekta binafsi kwani ni wadau wao wakubwa.
“Nyie ni wadau wa kubwa sana katika serikali,
mkituzalishia mabomba kwa wakati, yenye ubora yenye gharama halisi sisi kwetu hatutakuwa kikwazo,” amesema.
Ameongeza; “Sekta hii ya maji, nimekuwa karibu miaka mitatu naifahamu, hii wizara vilikuwepo visingizio kwa wataalamu wetu kwamba uzalishaji sijui nini ila kwa hali hii tuliyoiona, uzalishaji wa mabomba hususan katika utekelezaji wa miradi ya maji isiwe kisingizio,” alisema.
Baada ya kutembelea viwanda viwili kikiwemo cha Simba Plastick na Plasco, alionyesha kuridhishwa na uzalishaji wake hivyo ameagiza sh. bilioni moja zilipwe kwa kiwanda cha Simba Plastick, ambacho kimepewa kazi ya usambazaji wa mabomba katika mradi wa Kyaka-Nyakanazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo amevitaka viwanda hivyo kuongeza uzalishaji ili uweze kwenda na kasi ya utekelezwaji wa miradi katika maeneo ya vijijini nchi nzima.
More Stories
Serikali kuwezesha CBE kuwa kituo mahiri
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA
Mwanafunzi apoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba