November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri atoa agizo kukamilika ujenzi miundombinu ya madarasa

Daud Magesa na Judith Ferdinand, Mwanza

MBUNGE wa Jimbo la Ilemela,Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula,amekagua miradi ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa na kuagiza kasi iongezwe ikamilike kwa wakati.

Hayo aliyasema jana wakati alipotembelea miradi hiyo ya ujenzi kwenye kata 12 na kuridhishwa na maendeleo ya vyumba hivyo vya madarasa 97 vinavyojengwa kwa gharama ya bilioni 1.84 zilizokwishapokelewa kati ya bilioni 1.94.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewasaidia wananchi na kuwapunguzia mzigo wa michango ya ujenzi wa madarasa baada ya kutoa fedha hivyo Watanzania na wananchi wa Ilemela hawana budi kumshukuru na kupongeza kwa uamuzi huo wa busara lakini pia wanapaswa kushiriki ujenzi wa madarasa kwa vitendo ili ubora na thamani ya fedha ionekane.
Akiwa katika shule ya Sekondari Shibula, Dkt. Mabula alikumbana na changamoto ya baadhi ya wajumbe wa kamati wakiwemo viongozi wa CCM kususa kushiriki ujenzi hadi walipe posho kinyume na miongozo ya fedha za ujenzi wa madasara.

Amesema haiwezekani wananchi,wajumbe na viongozi wa Kata ya Shibula,washindwe kushiriki ujenzi wa madarasa hadi walipwe posho wakati maeneo mengine wamefanya na kuhoji kwa nini wagome baada ya serikali kuleta fedha za ujenzi wa madarasa.

“Rais Samia ametusaidia sana,ametuepusha na kero ya michango na tunapaswa kujiongeza na kuongeza kitu cha ziada kwa kutumia fedha hizo hizo, bila hivyo mwisho wa siku tutarudi kukamata kwa michango,fedha hizi ni za Rais, CCM kinatakiwa kisimamie miradi hii iende,”amesema Dkt.Mabula na kuongeza;

“Hivi serikali ina fedha za kuwalipa wote hapa? mmeletewa fedha za vyumba sita halafu bado mnataka posho,mnapaswa kujitolea nguvu zenu ili fedha zinazookolewa zifanye kazi nyingine za kuondoa changamoto za ziada na itakuwa ajabu serikali inaleta fedha mnagoma maana yake mnapuuza mchango wa Rais Samia.”

Akikagua ujenzi wa madarasa ya Kilimani Sekondari,Mbunge huyo wa Ilemela alisema imekuwa mbele kwa kila jambo na shule ya mfano kitaaluma jimboni humo ambapo kwenye ujenzi wa madarasa imekamilisha kwa asilimia 95.

“Mmeonesha mlivyo makini kwa kazi zenu, kwenye ujenzi mmekuwa wa kwanza kupapua na ndiyo maana perfomance yenu ya maendeleo na taaluma iko juu.Kwa juhudi hizo niwapongeze kamati,uongozi wa shule,jamii na wananchi,endeleeni na tutaendelea kuwaunga mkono,”amesema Dkt.Mabula.
Aidha aliziagiza kamati zote za ujenzi kuendelea kushirikiana ili madarasa yakamilike kwa wakati, kwa ubora kulingana na thamani ya fedha na kuwezesha kuondoa mrundikano wa watoto darasani na kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha sh. 1.84 kati ya 1.94 za kujenga madarasa 97 kwenye Jimbo la Ilemela.

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Diwani wa Kata ya Sangabuye,Renatus Mulunga,amesema maendeleo ya ujenzi wa madarasa kwenye manispaa hiyo ni mazuri na kutahadharisha kila senti itafanya kazi iliyokusudiwa.

Wakuu wa shule za Kilimani,Gerena Majaliwa,Lukobe Prosper Muyanja,Kisendi Khalid Kazinja na Shibula Michael Paul walieleza kukabiliwa na changamoto ya maji ya ujenzi na mabadiliko ya bei za baadhi ya vifaa.

Pia kukamamilika kwa madarasa walisema kutapunguza msongamano wa wanafunzi na kuwapa fursa ya kusoma kwa uhuru pamoja na walimu kufundisha katika mazingira bora na kuipongeza serikali kwa kuwapunguzia upungufu wa miundombinu ya madarasa.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula, akizungumza na baadhi ya wajumbe wa kamati za ujenzi wa shule ye Shibula jana alipokagua maendeleo ya mradi huo unaodaiwa kusuasua kutokana na wajumbe baadhi kususa wakishinikiza walipwe posho.

Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dkt. Angeline Mabula, akishiriki ujenzi wa shule ya sekondari Shibula jana.
Mmoja wa mafundi akimwangalia Mbunge wa Jimbo la Ilelema, Dkt. Angeline Mabula akichanganya saruji na mchanga aliposhiriki ujenzi wa shule ya sekondari Bugogwa jana.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula,akianglia na kusom ramani ya ujenzi wa shule ya Kilimani sekondari jana,kushoto ni Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga na kulia wa kwanza ni Katibu wa Mbunge huyo Kazungu Idebe kabla ya kukagua ujenzi wa mradi huo jana.

Waandishi wa habari wakifanya mahojiano na Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dkt. Angeline Mabula baada ya kukamilisha ziara ya kugagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa katika kata 12 kati ya 19 za jimbo hilo jana.
Picha zote na Daud Magesa na Judith Ferdinand.