November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri ahimiza wananchi kutunza mazingira

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amehimiza wananchi kuendelea kulinda na kutunza mazingira na kuhifadhi maeneo ya vyanzo vya maji.

Kauli hiyo imetolewa katika ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kijiji cha Mkoleko Jimbo la Kibakwe Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.

“Tuanzishe mradi wetu wa maji kupitia vyanzo vya maji tulivyonavyo kwenye Mlima, ili tupate maji ya uhakika kwa ajili ya shughuli za kijamii.”

Aidha watendaji wa kata muendelee kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi ,ikiwa ni sambamba na kutunga sheria ndogo ndogo ili kuzuia ukataji wa miti katika kingo za makorongo ili kuzuia mmonyoko.

“Kama una miti pembezoni mwa shamba lako iache usiikate ili iendele kuzuia mmonyoko wa ardhi, inayoharibu miundo mbinu ya barabara.”

Waziri Simbachawene ameahidi kuendelea kuimarisha barabara zinazounganisha vijiji vyote vinavyounganisha kata ya Mansa kwa kuhakikisha barabara hizo zinafanyiwa ukarabati katika maeneo korofi.

Akimkaribisha Waziri, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpwapwa Mhe. Richard Maponda amemshukuru Waziri Simbachawene kwa jitihada zake za kuleta maendeleo katika Halmashauri ya Mpwapa, kuna zahanati sita zimefunguliwa na watu wanapata dawa.

“Kuna shule zimepata usajili ambazo zitasaidia kutatua adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.”

Naye Bwn. Emmanuel Nzoka ameshukuru serikali kupitia kwa mbunge kwa kutengeneza barabara na kuwa katika hali nzuri katika majira yote ya mwaka.

“Tulikuwa kisiwani kutokana na barabara kuharibika kutokana na maji ya mvua hivyo kushindwa kupitika katika majira ya masika.”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akizungumza na wananchi katika Mkutano wa aliofanya katika Kijiji cha Mkoleko.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alipotembelea boma la nyumba ya walimu katika shule ya Msingi Makose
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alipotembelea zahanati ya Winza.