November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri aahidi kupambana na wanaomkwamisha Samia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Ashatu Kijaji, ameahidi kuwaondoa watumishi watakaokwamisha shughuli za uwekezaji kwa urasimu.

Amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuhakikisha wawekezaji wanataka vyeti vya tathmini ya athari ya mazingira (EIA) wanapata ndani ya mwezi mmoja.

Ameyasema hayo jana alipotembelea ofisi za baraza hilo Mikocheni kuzungumza na wafanyakazi wa baraza hilo na kuwapa maelekezo ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

Amesema hatafurahi kuona wawekezaji wanazungushwa kupata vyeti hivyo vitakavyowasaidia kuanza uwekezaji wao na kwamba mtumishi atakayejaribu kuwakwamisha basi atakutana na adhabu kali kutoka kwake.

Dkt. Kijaji amesema Rais Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada kubwa kutafuta wawekezaji maeneo mbalimbali duniani hivyo atashangaa kuona wasaidizi wake wanawakatisha tamaa wawekezaji hao kwa urasimu.

“Mimi sitakubali kuwa sehemu ya kukwamisha juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutafuta wawekezaji wanaokuja kuwekeza hapa nchini, tuweke muda mtu akiomba cheti hata siku 30 tuwe tumetoa na mwekezaji akaanza kufanyakazi, kama ananyaraka zote kwanini tumkwamishe,” alisema

Amesema mtu anayejaribu kukwamisha wawekezaji wanawakwamisha watanzania kwani mwekezaji anapoweka mradi anatengeneza ajira kwa wananchi na kuongeza kuwa hata kama ana upungufu basi NEMC ndiyo yenye mamlaka ya kumsaidia kurekebisha.

“Wawekezaji wengi wanakopa benki wanakuja kuwekeza mnawakwamisha sasa jiweke kwenye nafasi hiyo, kama inawezekana mwambie inaweekana na kama haiwezekani mwambie haiwezekani lakini siyo kumzungusha kila siku mpaka anachoka,” amesema

“Kwa bahati nzuri mimi huwa nafuatilia sana na ntahakikisha yeyote anayejaribu kukwamisha mwekezaji nitamshughulikia na hata huko nilikotoka nimewashughulikia sana watu. National Development Corporation (NDC) lilikuwa inakaribia kufutwa kwa kufanya vibaya lakini niliwanyoosha mpaka sasa imesimama baada ya mimi kuwanyoosha,” amesema

Ameitaka NEMC kusimamia sheria na kuhakikisha mifuko ya plastiki hairejee tena kwenye matumizi kwani wananchi wanalalamika kwamba mifuko hiyo hivi sasa imejaa masokoni kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Nikiwa kwenye mkutano huu huu nimetumiwa ujumbe na mwananchi analalamika kwamba mifuko hii imejaa kila kona lakini sisi tupo kwanini tusichukue hatua kwa wazalishaji wake. Kama ilizuiwa kwanini inarudi tena wakati sheria zipo na tuliipiga marufuku,” mesema Waziri