September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee waomba kupatiwa huduma ya kliniki ya mkoba

Na Esther Macha,TimesMajira Online. Mbarali

WAZEE wilayani Mbarali Mkoa Mbeya, wameiomba serikali kuwapatia huduma ya kliniki ya mkoba kwa kata na vijiji, ambako hakuna vituo vya afya japo mara moja kwa mwezi wakati wakisubiri kujengewa zahanati na vituo vya afya .

Wamesema wazee wengi hawana uwezo wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu kutokana na hali duni walizokuwa nazo, pamoja na kuwa na umri mkubwa.

Hali hiyo pia inasababisha wazee wengi kutokwenda hospitali kabisa na hivyo kupoteza maisha kwa kukosa tiba kutokana na kushindwa kuvifikia vituo vya afya ambavyo vipo umbali mrefu.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Baraza la Wazee Wilaya ya Mbarali, Hezron Kapwela wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani ambayo kiwilaya yalifanyika katika Kata ya Ubaruku.

Pia wamesema kuna upungufu wa dawa muhimu za wazee katika zahanati, vituo vya afya na Hospitali ya Wilaya hali inayowafanya wazee wengi kukosa huduma za matibabu.

Hata hivyo, Kapwela amesema wanaomba ugawaji wa dawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali uzingatie mahitaji ya wazee.

Katibu huyo amesema, wazee ambao hawana uhakika wa mlo, mavazi yao yamechaka na hawana wategemezi wameziomba halmashauri za wilaya wawakilishi pamoja wawakilishi wao ambao ni Madiwani, Wabunge, mashirika, wahisani na jamii kuangalia kundi hilo kwa sababu msaada wanaohitaji ni mkubwa.