January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee wakumbushwa kukemea mmomonyoko wa maadili

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Baraza la Taifa la Wazee limeaswa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kurekebisha na kusimamia maadili mema ya Taifa.

Rai hiyo imetolewa Desemba 04, 2023 na Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii, Tulo Masanja alipomwakilisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, kwenye ufunguzi wa kikao cha siku mbili cha Baraza la Wazee la Taifa kililofanyika jijini Dodoma.

Kamishna Masanja amesema kuwa Serikali inawathamini wazee na itaendelea kupokea ushauri wao wa busara kwa ustawi na maendeleo ya nchi.

“Niombe sana Baraza hili lichukue nafasi yake kama washauri wa jamii kwa kukemea yale yote yanayosababisha ukatili, unyanyasaji, unyanyapaa, mauaji pamoja na mmomonyoko wa maadili katika jamii” amesema Kamishna Masanja.

Kamishna Masanja amelitaka Baraza hilo kuendelea kufanya kazi kwa kushirikana na wadau wengine wanaoweza kutekeleza afua mbalimbali za wazee kwani Baraza hilo limeundwa kwa mujibu wa sheria hivyo ni vema taasisi nyingine zote kuhakikisha zinatumia mifumo iliyopo kwa maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Albina Chuwa amesema kuwa Baraza la Wazee la Taifa ni hazina ya msingi na ni tunu ya Taifa kwa hivyo wanayo kila sababu ya kutekeleza kila afua zitakazolisaidia taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo David Sendo amesema kuwa Baraza hilo litahakikisha linasimamia na kutekeleza maazimio ya kikao hicho ikiwa ni pamoja na kufutilia afua mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazohusu kundi la wazee nchini.

“Shabaha yetu ni kufuatilia kikamilifu na kusimamia upitishwaji wa Sera mpya ya Wazee nchini ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa katika mchakato bila mafanikio kwani sisi wazee tunahitaji huduma Bora za Afya na mazingira wezeshi kwa wazee kushughulikiwa ipasanyo” amesema Sendo.