November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi watakiwa kuwekeza kwenye elimu kwa ustawi wa watoto

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Chunya

KATIKA kuhakikisha watoto wanakuwa na elimu bora wazazi na walezi  Jijini Mbeya wameaswa kuendelea kuwekeza katika elimu ambayo ndiyo nguzo kuu kwa maisha yao .

Hayo yamesemwa na Mdau wa maendeleo Jijini Mbeya ,Titoth Tweve wakati wa mahafali ya kwanza ya darasa la saba ya shule ya awali na msingi Holy Land ya Makongolosi Wilayani Chunya inayomilikiwa na Lawena Nsonda (Baba mzazi .

Tweve amesema kuwa wazazi wanapaswa kuweka kipaumbele suala la elimu kwa watoto na kuwa sehemu ya kuwekeza kwao kwenye Elimu .

“Elimu ndiyo urithi pekee kwa watoto wetu hivyo ni vema wazazi wenzangu tuendelee kuwekeza na kuweka kipaumbele suala la elimu kwa watoto wetu maana huu ni urithi pekee ambao ndiyo zawadi kuu kwa watoto wetu ,zawadi pekee kwa watoto ni elimu hivyo tujitoe kadri ya uwezo wetu tuache alama”amesema Tweve.

Hata hivyo  Tweve katika mahafali hayo amechangia tani tano za saruji zenye thamani ya shilingi  mil.5 kwa ajili ya ujenzi wa uzio ili  kuimarisha usalama wa watoto katika shule hiyo.

Aidha Tweve ameupongeza uongozi wa shule ya Holly Land Pre and Primary School kwa namna ilivyojikita katika kutoa elimu bora hali iliyowafanya wazazi kutoka maeneo mbalimbali nchini kuwaleta watoto shuleni hapo.

Awali Mwalimu Mkuu wa shule ya Holly Land, Yona Mwakalinga amesoma taarifa ikionesha mafanikio tangu kuanzishwa ambapo ilianza na watoto wawili lakini kwa sasa ina watoto zaidi ya 600.

Mwakalinga amesema shule imekuwa na muendelezo mzuri wa matokeo ya darasa la nne Kiwilaya,Kimkoa na Kitaifa ambapo matokeo ya mwaka 2021 mtihani wa darasa la nne Kitaifa shule ya Holly Land iliongoza.

Mkurugenzi wa Holy Land Lawena Nsonda  (Baba mzazi )amesema ushirikiano uliopo baina yake,walimu, watumishi na wanafunzi ndiyo siri ya mafanikio.

Pia malipo ya mishahara kwa wakati na motisha mbalimbali umefanya watu wote kufanya kazi kwa bidii hivyo kuongeza ufaulu wa wanafunzi na matarajio ni kufanya vizuri zaidi mtihani wa darasa la Saba.

Lawena Nsonda ameahidi wanafunzi wanaohitimu mwaka huu wakiongoza Kitaifa atawapeleka Dubai kwa ajili ya mapumziko.

Lawena Nsonda amesema awali wanafunzi walioongoza mtihani wa darasa la nne aliwapeleka mapumziko Jijini Dar es Salaam na Zanzibar kwa usafiri wa ndege.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa shule ya Holly Land ambaye ni mke wa Lawena Nsonda,Winfrida Lawena amesema mumewe ni mlezi wa watoto hivyo inafanya kutekeleza kila huduma kwa watoto hali iliyowafanya wazazi kupenda kuwaleta watoto na watoto kupenda masomo.

“Baadhi ya watoto shule ikifunga wengi wao hawapendi kwenda nyumbani kutokana na malezi bora ya watoto kutoka kwa walimu”amesema mke wa Lawena.

Wadau mbalimbali waliohudhiria mahafali hiyo wamemuunga mkono kwa kuchangia fedha ili kukamilisha wa uzio.