January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi watakiwa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge amewataka wazazi wenye ulemavu wasiwafiche bali wawapeleke shule kupata elimu kama watoto wengine kwani kuwa na mtoto mwenye ulemavu sio laana bali ni baraka.

Lakini pia alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Lushoto na kutembelea wodi ya mama na mtoto, alitoa fedha ili kuwakatia bima ya afya wanawake wanane (8) waliokuwa wamejifungua na wanaotarajia kujifungua akiwemo mwanamke aliejifungua watoto watatu njiti ambapo pia alimpa sh. 50,000 ili akaanzie kununua vitu vidogo vidogo vya watoto.

Akizungumza Julai 22, 2024 mara baada ya kufika Shule ya Msingi Lwandai, Kijiji cha Mlalo, Kata ya Mlalo, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ili kuwaona wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ambapo Serikali imewajengea darasa la kipekee lenye kila kitu, amesema na wao wanahitaji kupata elimu.

“Wazazi wasiwafiche watoto wenye ulemavu wa aina yeyote ile, bali wanatakiwa kuwatoa na kuwapeleka shule ili wapate elimu kama ilivyo kwa watoto wengine, nataka kuwaambia ndugu zangu, mtoto kuwa mlemavu sio laana bali ni baraka, hivyo mnatakiwa kuwapeleka shule nao wapate elimu.

“Watoto wenye usonji, nyuma yake kuna baraka kubwa, hivyo tuwaenzi na kuwaona ni watu ambao wakipata elimu wataweza kumudu maisha yao, na kuweza kuwasaidia wengine,nimesikia kuna mahitaji yanatakiwa, lakini mimi nataka kuanza kwa kutoa Bima ya Afya kwa hawa watoto 30 waliopo kwenye hili darasa, watakaa kama familia sita sita ili kutengeneza familia tano ambazo zitapatiwa matibabu” amesema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge amesema moja ya mahitaji ya watoto hao ni kujengewa bweni ili waweze kuishi hapo hapo shuleni, lakini pia kupatiwa walimu kwani hadi sasa hawana mwalimu hata mmoja mwenye taaluma ya elimu maalumu.

Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lwandai Nasibu Muya, amesema shule yake ina jumla ya vitengo vitatu, Elimu Msingi darasa la awali hadi la saba, Kituo cha Elimu Ufundi, na Kituo cha Elimu Maalumu, ambapo Kituo cha Elimu Maalumu kina wanafunzi 30, wavulana wakiwa 18 na wasichana 12 ambao wana aina tofauti za ulemavu ikiwemo usonji, viungo na akili.

“Katika mafanikio, wapo wanafunzi watano waliokamilisha hatua  zote tatu za ujifunzaji katika kitengo na stadi mbalimbali, na kuweza kuandikishwa elimu msingi, ambapo hadi sasa wapo wanafunzi wanne wanasoma darasa la nne, wavulana watatu na msichana mmoja wa darasa la tatu. Na Serikali imewajengea darasa moja na matundu matatu ya vyoo kupitia Mradi wa BOOST 2022/2023 na wanapata chakula cha mchana shuleni kwa ruzuku ya Serikali.

“Kitengo hiki kina changamoto ikiwemo ukosefu wa walimu wenye taaluma ya uhitaji maalumu na baadhi ya wanafunzi kutofika shuleni kwa wakati kutokana na umbali na changamoto za ulemavu wao, Lakini mapendekezo yetu, kituo kijengewe mabweni kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu uliozidi ili wapatiwe  huduma muda wote” amesema Muya.

Pia alipofika Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Chanika na Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Mkata, alitembelea wodi za mama na mtoto, na kutoa fedha ili wanawake wajawazito 10 waliolazwa wakisubiri kujifungua na waliojifungua wakisubiri kupata nguvu, aliwakatia bima ya afya.

Akiwa Shule ya Sekondari Rashid Shangazi iliyopo Kata ya Mlalo aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kurudisha fadhila kwa Serikali, kwani imejenga miundombinu ya madarasa na nyumba za walimu kwa fedha nyingi, hivyo ni lazima waoneshe uzalendo kwa kusoma kwa bidii, huku wakiziishi ndoto zao, huku wakitakiwa kujifunza kwa waliofanikiwa.

Katika tukio jingine, Mhandisi Ulenge ametoa sh. 600,000 kama mchango wake kwa Msikiti wa Kijiji cha Mavumo, Kata ya Shume wilayani Lushoto kwa ajili ya kununua saruji tani mbili ili kukamilisha ujenzi wa msikiti huo.