Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Katika kuhakikisha changamoto ya idadi ya watoto wanaokimbilia kuishi na kufanya kazi mtaani inapungua,wadau mbalimbali mkoani hapa wametakiwa kuwaelimisha wazazi umuhimu wa mtoto kwenda shule.
Huku Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo mkoani Mwanza,wameadhimia kufanya operesheni ya miezi kwenye mitaa itakayoenda ambamba na kuwaondoa watoto wanaozagaa mitaani na kuhakikisha wanarudishwa shuleni.
Hayo yamesema na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike,wakati Akizungumza kwenye kikao kazi cha kamati ya kupambana na Ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) ngazi ya Mkoa ambacho kililenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuwaondoa watoto mitaani na kutokomeza utoro mashuleni kilichofanyika mkoani hapa mwishoni mwa wiki iliopita.
Samike amesema,ili kukomesha changamoto hiyo wadau wanapaswa kuwasaidia wazazi kupata elimu ya umuhimu wa mtoto kwenda shule jambo litakalosaidia kupunguza idadi ya watoto wa mitaani.
Amesema serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya elimu bila malipo ambapo hivi karibuni Mkoa wa Mwanza ulipokea kiasi cha bilioni 20.5 kwa ajili ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati hivyo si vyema watoto wakakosa haki ya kupata elimu.
Hivyo katika mpango huo jambo la muhimu ni kuwaelimisha wazazi wasiwe chanzo cha watoto kuwa mitaani kwa sababu tatizo lililopo ni wazazi kuwa chambo kwa watoto wao katika kuwapanga na kuwafundisha maneno ya uongo ya kusema na wanapofuatiliwa huwahamishia sehemu nyingine.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza, Isack Ndassa amesema zaidi ya asilimia 90 ya watoto walio mitaani wana umri wa kwenda shule lakini wanakosa haki ya kupata elimu kutokana na sababu mbalimbali.
Akitoa taarifa ya hali ya utoro katika shule za msingi na sekondari mkoani Mwanza, Kaimu Afisa Elimu watu wazima na elimu ya mfumo, Maenda Chambuku,amesema utoro ni sehemu ya watoto waliopo mitaani hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha wanawaelimisha wazazi waweze kupunguza tatizo hilo.
Hivyo ameeleza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Aprili mwaka huu jumla ya wanafunzi ambao ni watoro 19,133 wameripotiwa shule ya msingi huku shule ya sekondari ikiwa ni wanafunzi watoro 7,594.
Amesema serikali imeweka mifumo rafiki kwa wanafunzi ambao hawako shuleni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba na utoro kurejea shuleni hivyo jitihada zifanyike ili kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya kwenda shule.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Kivulini, Yassin Ally amesema changamoto ya watoto mitaani inachangiwa na suala la utoro mashuleni.
Hivyo walimu wanapaswa kuwa na mbinu rafiki kwa wanafunzi za ufundishaji ikiwa ni pamoja na kupunguza adhabu kali kutokana na kukosa sare za shule au kufeli mitihani.
Sanjari na hayo Yassin ameeleza kuwa tathimini iliyofanyika mwaka 2017 na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa mikoa sita inaonesha Jiji la Mwanza ni la pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wa mitaani waliokadiriwa kufikia 978 huku Mkoa wa Dar-es-Salaam ukiongoza kwa kuwa na watoto wengi ambapo jumla ni 2,684,Iringa 954, Mbeya 586 na Dodoma 346.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi