Na David John, Timesmajira Online
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Kilombero Saidi Mrisho ametoa wito kwa wazazi kuchangia huduma ya chakula mashuleni kama inavyoelekeza Mwongozo wa Kitaifa ya Utoaji Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimu msingi wenye lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa elimu nchini.
Amesema wazazi ni kiungo muhimu katika maendeleo ya watoto wawapo mashuleni na mpango wa utoaji huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi utachochea kuacha tabia za utoro kwa wanafunzi hususani shule za vijijini.
Mwenyekiti huyo ameyasema hayo katika mwendelezo wa ziara ya kamati ya utekelezaji Jumuiya ya Wazaji CCM katika shule za Wazazi (TAPA) Kilombero amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 imetamka wazi kuwa utoaji wa huduma muhimu kama chakula bora, maji safi na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanafunzi wawapo shuleni ni muhimu.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano awamu ya Sita Chini ya Dokta Samia Suluhu Hassani imeandaa Mwongozo wa kisera ili kuweka utaratibu wa Kitaifa utakaonufaisha shule na wanafunzi wote wa Elimu msingi, hivyo wazazi mna wajibu mkubwa kushiriki kikamilifu katika kusimamia suala hilo kwa watoto.
Mrisho amesema mwanafunzi anapokosa chakula shuleni anaweza kupata madhara ikiwemo kukosa usikivu wakati wa ujifunzaji, mahudhurio hafifu yanayopelekea utoro na hata kukatisha masomo na kushuka kwa ufaulu.
“Natambua kwamba utoaji wa huduma ya chakula na lishe ni suala mtambuka linalohitaji ushiriki wa sekta na wadau mbalimbali. Ni matumaini yangu kuwa kila mzazi atashiriki kuhakikisha anashirikiana na shule zetu na kutekeleza majukumu yake ipasavyo,” amesema Mrisho
Aidha Mrisho ametoa rai kwa idara zote za Serikali na Wizara zinazohusika na jukumu hili kuhakikisha zinasimamia utekelezaji wa Mwongozo huo na kutoa wito kwa wadau wote wa Elimu kushiriki, kuchangia kwa hiari na upatikinaji wa chakula chakula bora kwa watoto wanapokuwa shule
“Niwaombe wadau wetu wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni binafsi na vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha ili kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata chakula wanapokuwa shuleni,” amesisitiza
Akiongea katika ziara hiyo Magret Haule ameiomba Halmashauri ya Kilombero na Serikali za vijiji kutekeleza sulala huduma za chakula shuleni kuendelea kutoa huduma hiyo kwa kuzingatia Sera iliyopoAmeongeza kuwa mpango huo umeongeza uelewa wa wazazi katika kuchangia chakula shuleni.
Amesema pamoja na juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji, hakutakuwa na matokeo tarajali kama litasahaulika suala la upatikanaji wa chakula bora kwa wanafunzi wawapo shuleni.
More Stories
Dodoma yaandaa Kongamano kutatua changamoto za ajira kwa vijana
Dkt. Pindi Chana aweka jiwe lamsingi jengo la jiolojia Karatu
TotalEnergies yampongeza Rais Samia maboresho kwenye elimu