December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi washangazwa umahiri wa kingereza wanafunzi Tusiime.

Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Abdul Maulid akimpa cheti mmoja wa wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu darasa la saba kwenye shule ya Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam kwenye mahafali yaliyofanyika leo shuleni hapo. Anayefuata ni Mwenyekiti wa Bodi ya shule, Jonson Kapira na Mkurugenzi wa shule za Tusiime, Dk. Albert Katagira.
Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Abdul Maulid akikata keki na wanafunzi wa darasa la saba wa shule ya Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam kwenye mahafali yaliyofanyika leo shuleni hapo.
Wanafunzi wa shule ya msingi Tusiime wakiigiza igizo la Sinderera wakati wa mahafali ya 19 shuleni hapo.
Mkurugenzi wa shule za Tusiime, Dk. Albert Katagira akihojiwa na mtangazaji wa kituo cha televisheni ya ya shule hiyo wakati wa mahafali ya 19 ya shule ya msingi yaliyofanyika shuleni hapo.
Wanafunzi wa shule ya msingi Tusiime ya Tabata Dar es Salaam wakijiandaa kutumbuiza kwa igizo maalum wakati wa mahafali ya 19 yaliyofanyika shuleni hapo.

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

UMAHIRI wa hali ya juu wa kumudu kuzungumza lugha ya kingereza kwa ufasaha ulioonyeshwa na wanafunzi wa shule ya msingi Tusiime umemfurahisha Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Abdul Maulid na kuwaduwaza wazazi waliohudhuri mahafali yao.

Maulid mgeni rasmi kwenye mahafali ya 19 ya shule hiyo ambayo yamefanyika leo shuleni hapo Tabata jijini Dar es Salaam kwa wanafunzi kuonyesha umahiri wao kwenye maigizo mbalimbali kwa lugha ya kingereza.

Mbali na mgeni rasmi wazazi nao walionekekana kupigwa na butwaa kutokana na namna wanafunzi hao wa shule ya msingi walivyoweza kumudu kuzungumza lugha ya kingereza kana kwamba wako vyuo vikuu.

Igizo lililowakuna wengi akiwemo mgeni rasmi na wazazi wa wanafunzi hao ni lile ambalo mmoja wa wanafunzi wanaohitimu kuigiza kusoma taarifa ya habari kwa lugha ya kingereza bila kutetereka.

Kwenye taarifa hiyo ya habari Mwanafunzi mwingine wa darasa la tano alionyesha uwezo mkubwa wa kufanya uchambuzi hali ambayo iliwafanya wazazi wengi kubaki na mshangao.

Akizungumza kwenye mahafali hayo, Maulid aliwapongeza walimu wa shule hiyo na Mkurugenzi wa shule hizo, Dk. Albert Katagira kwa namna walivyoweza kuwaandaa wanafunzi hao kitaaluma na wengine kuzungumza kingereza kama wamezaliwa nacho.

“Nimewasikiliza wanafunzi wanavyozungumza kingereza kwenye masuala mbalimbali kwa kweli wazazi mtaungana namini kusema kwamba hamkukosea kuleta watoto wenu hapa Tusiime, binafsi nimeshangazwa na umahiri wa wanafunzi hawa huwezi kuamini kwamba wako shule ya msingi,” amesema Maulid na kuongeza

“Kwenye taaluma mmekuwa mkifanya vizuri mwaka hadi mwaka na leo nimeona kitu kingine hapa. Lugha ya kingereza imenyooka si mchezo kwa kweli walimu mnajitahidi sana endeleeni na moyo huo,” amesema Maulid

Mmoja wa wazazi aliyekuwa kwenye mahafali hayo, Antony Nazael amesema siku ya leo ameshuhudia mambo ambayo yamemshangaza kwani hakutarajia mwanafunzi wa shule ya msingi anaweza kuwa mahiri kwa kiwango alichoona

“Mwanafunzi aliyesoma taarifa ya habari kwa lugha ya kingereza mtu anayesikiliza anaweza kudhani kwamba ni taarifa ya habari kweli kutokana na lugha nzuri ya kingereza na mpangilio mzuri kumbe ni maigizo tu. Nawapongeza walimu wamefanyakazi kubwa sana kuwapika,” amesema

Mzazi mwingine, Kassim Jumbe alisema mwanafunzi aliyefanya uchambuzi wa masuala mbalimbali ya michezo yanayoendelea nchini ikiwemo Ligi Kuu ya Uingereza kwa lugha ya Kingereza ameifanya siku yake kwenda vizuri kwani ameonyesha kipaji cha aina yake.

“Yule mwanafunzi atakuwa mchambuzi mahiri sana wa michezo siku za usoni nimemsikiliza vizuri amenofurahisha sana na hivi ndivyo vipaji ambavyo tunapaswa kuvilea na kuviendeleza kama alivyosema mgeni rasmi,” amesema