January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi zingatieni lishe bora ya watoto shuleni

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Diamanda Foundation ,Dimanda Kaphipa amewaasa wazazi kuzingatia lishe kwa watoto shuleni na nyumbani ili kuondoa ukatili wa lishe kwa watoto.

Kaphipa ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa hafla ya kutoa uji wa lishe kwa watoto kuanzia darasa la awali hadi darasa la nne katika shule ya msingi Makulu .

“Leo tumekuja kwa ajili ya kutoa elimu kwa wazazi kuhusu lishe kwa watoto hasa shuleni,lakini pia tumekuja na uji wa lishe bora na wenye virutubisho vyote ili wazai nao waige mfano huo.”amesema Kaphipa

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Lishe bora na huduma zingine za msingi kama elimu na afya ni haki ya kila mtoto ikimaanisha kuwa watoto wote wana haki ya kupata elimu pamoja na lishe bora yenye virutubisho ili kusaidia ukuaji wa mwili,kiakili ,kuondokana na udumavu unaotokana na lishe duni na hatimaye kufikia katika utimilifu wake.

Kaphipa amesema,kuna idadi kubwa ya watoto hukosa haki hususan lishe bora kutokana na sababu mbalimbali za familia ukiwemo umasikini wa kipato hali ambayo husababisha watoto kutopenda shule ,kufanyiwa vitendo vya ukatili ,kuwa na ufaulu mdogo darasani ,kupata magonjwa ya mara kwa mara na kusababisha utapiamlo.

“Mtoto akiwa na njaa anakuwa dhaifu hawezi akasoma kwa ufanisi kutokana na kukosa lishe inapelekea mahudhurio yake shuleni kuwa hafifu ,lishe bora inajenga afya na akili, hivyo watoto wakipata  chakula shuleni na asubuhi kabla hajaenda shuleni itapunguza utoro shuleni lakini pia itapunguza vitendo vya ukatili.”amesema Kaphipa

MKURUGENZI Mkuu wa Diamanda Foundation ,Dimanda Kaphipa akizungumza katika hafla ya ugawaji uji wa lishe wenye virutubisho vyote wa mfano katika shule ya msingi Makulu jijini Dodoma.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimwer amesema,wazazi wanakosea kutumia muda mwingi kutafuta maisha huku malezi ya watoto yakiyaweka kando hali inayosababisha changamoto nyingi kwa mtoto na hivyo kushindwa kufikia ukuaji timilifu.

“Suala la ulezi ni jukumu muhimu na suala la utafutaji linafuata,lakini siku hizi wazazi wameweka mbele zaidi suala la kutafuta pesa ,wamewasahau watoto na kuwaacha na wasichana wa kazi ambao hawana uelewa wowote kuhusu suala la lishe ya mtoto na hivyo kuwasababishia ukatili wa kukosa lishe bora.”amesisitiza Kimweri

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wa Makulu Anthony John Mkazi wa Makulu amesema,elimu waliyoipata kuhusu lishe kutoka kwa Dimanda Foundation imewafumbua macho huku akionyesha utayari wa kuhakikisha anazingatia suala hilo kwa watoto nyumbani pamoja na shuleni.

Christina Haule mwanafunzi wa shule hiyo ameishukuru taasisi hiyo ya Dimanda Foundation kwa kutoa uji kwa watoto lakini kubwa zaidi ni kuhimiza wazazi kuzingatia lishe kwa watoto jambo ambalo amesema litasaidia watoto kuwa na usikivu darasani .

Akizungumza na Mtandao huu,Afisa Lishe wa Jiji la Dodoma Semeni-Eva Juma ,Takwimu za mwaka 2016 za wilaya ya Dodoma zinaonyesha asilimia 41 ya watoto wamedumaa ikimaanisha kuwa, kati ya watoto 100 ,watoto 41 lishe zao ni duni sana huku Kimkoa takwimu zinaonyesha asilimia 37.2 ya watoto wamedumaa ikimaanisha kuwa katika watoto 100,watoto 37 wamedumaa yaan hawakupata lishe bora .