December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi Tusiime waduwazwa na vipaji vya wanafunzi wa chekechea 

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online 

WAZAZI walioshiriki siku ya taaluma na maonyesho ya shule ya awali Tusiime leo wameshangazwa na vipaji vilivyoonyeshwa na wanafunzi hao kwa kumudu kutengeneza vitu mbalimbali na kumudu kuzungumza kingereza fasaha muda wote.

Maonyesho hayo yaliyofanyika leo  kwenye shule ya Tusiime Tabata Sanene yamehusisha utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo shanga, chakula cha tamaduni za makabila mbalimbali, vifaa vya usafiri wa anga, kuonyesha tamaduni za kimasai, michoro ya vitu mbalimbali.

Wanafunzi hao pia walionyesha umahiri wa kutengeneza juice za aina mbalimbali hali ambayo iliwavutia wazazi na washiriki wengine wa maonyesho hayo.

Mwanafunzi aliyetia fora zaidi ni Vadim Dmitry ambaye alifanikiwa kuwaeleza wageni kuhusu namna ndege inavyotengenezwa, inavyoweza kuruka na kutua salama kwenye njia yake.

Mwanafunzi huyo alikuwa akitoa maelezo hayo kwa lugha ya kingereza bila kubabaika hali ambayo iliwavutia washiriki wa maonyesho hayo ya leo.

Mkuu wa shule hiyo ya awali, Pamela Mbonanibukya amesema umahiri wa wanafunzi hao haujaja kwa urahisi kwani ni kazi kubwa inayofanywa na walimu wa shule hiyo.

Amesema wamefanikiwa kuwa na walimu mahiri na wanaojituma kwenye kazi zao ambao wamekuwa wakiwaandaa wanafunzi kwaaajili ya kupata ujuzi mbalimbali utakaowasiaidia siku za baadae.

Amesema kupitia maonyesho hayo wamekuwa wakivumbua vipaji mbalimbali vya wanafunzi ambavyo kama vitaendelezwa vitawasaidia kuja kuwa watu wa kutegemewa sana kwenye jamii.

“Tusiime hatuna jambo dogo, hapa tumeanza na nakuhakikishia wanafunzi hawa watakuja kufanya mambo makubwa sana zaidi ya haya ambayo umeona leo kwasababu kuna mengi tumeandaa,” alisema mwalimu Pamela.