Na Magesa Magesa,Timesmajira Online. Arusha
WAZAZI na walezi Jijini Arusha, wametakiwa kuhakikisha
wanatambua na kutimiza majukumu yao kwa watoto kwa kuwapatia mahitaji yao muhimu kama malezi, mavazi na chakula lengo likiwa ni kuhakikisha ongezeko la watoto wa mitaani linatokomezwa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt. John Pima katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Ofisa Uchaguzi, Namnyak Laitetei katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto wa mitaani yaliyofanyika katika kituo cha kulelea watoto na vijana wa mitaani cha Amani kilichopo Kaloleni jijini hapa.
Amesema tatizo la ongezeko la watoto wa mitaani kwa kiasi kikubwa linachangiwa na wazazi na walezi, kushindwa kutimiza majukumu yao hivyo wakati umefika kwa kila mmoja, kuhakikisha anatimiza kikamilifu majukumu yake kwa kuwahudumia watoto hao ipasavyo.
“Jiji la Arusha tuna jumla ya watoto wa mitaani 544 kutokana na mfarakano wa kifamilia, watoto kunyanyaswa majumbani na mashuleni, umaskini pamoja na matatizo ya kinidhamu hali inayosababisha ongezeko kubwa la watoto wa mitaani,” amesema.
Ametoa wito kwa jamii kuacha mara moja kuwatumikisha watoto katika shughuli mbalimbali ikiwemo masokoni, mashambani na kuwatumia wao kuomba hela kwa watu wengine na kwamba yeyote yule atakayebainika, atachukuliwa hatua kali za kisherea.
Kwa upande wake Ofisa Vijana wa kituo hicho, Ally Mwanja amesema kituo kilianzishwa mwaka 2001 na kwamba kimekuwa kikiwahudumia watoto na vijana wa mitaani kwa kuwalea na kuwapatia mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kujiajiri.
“Mpaka sasa tumekwishatumia zaidi ya sh. milioni 165 kwa ajili ya kuwasomesha vijana hawa katika fani mbalimbali ikiwemo mapishi, urembo, ushonaji na uunganishaji wa umeme wa majimbani na kwenye magari na pindi wanapohitimu mafunzo hayo, tumekuwa tukiwakabidhi vifaa vya kufanyia shughuli zao,” amesema.
Mwanja ametoa wito kwa jamii, taasisi na mashirika mbalimbali kujitokeza kwa wingi katika kuwasaidia watoto hawa wa mitaani, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha kuwa ongezeko la watoto hawa wa mitaani linapungua kama si kumalizika kabisa.
Awali akisoma risala ya kituo hicho, Eliya Jonathan amesema katika maisha yao ya mitaani wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa, kunyanyaswa kingono, kubaguliwa kukosa huduma muhimu kama malazi, chakula na mavazi ikiwa ni pamoja na kuitwa majina mabaya na jamii.
Ameiomba serikali itenge bajeti kwa kuwawezesha watoto wanaoishi katika mazingira hayo, kupata mahitaji yao muhimu ikiwemo elimu kwani wao ni watoto kama walivyo wengine na hawakupenda kuishi kwenye mazingira hayo.
More Stories
Chunya yafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
HGWT yawarejesha kwao wasichana 88 waliokimbia ukeketaji
Sherehe Miaka 61 ya Mapinduzi Zanzibar zafana