January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi msifiche watoto wenye ulemavu wakati wa zoezi la Sensa

Na Esther Macha,Timesmajira,Online  Mbeya.
 
WAZAZI na Walezi nchini wametakiwa kutowaficha ndani watoto wao wenye ulemavu na badala yake wahakikishe wakati wa zoezi la Sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu nchini kote.
 
Wito huo umetolewa na Programu meneja wa kituo cha elimu jumuishi cha Child Support Tanzania(CST), Hildergade Mehrab wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto Afrika iliyofanyika Kimkoa katika viwanja vya Shule ya Msingi Nzovwe jijini Mbeya.
 
Amesema katika kuelekea kwenye kilele cha sensa kituo hicho kimejipanga kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii na walezi kwa ujumla kutowaficha watoto wenye ulemavu majumbani ili nao wapate haki ya kuhesabiwa.
 
Aidha Mehrad ameongeza kuwa tayari gari limepatikana la kuwezesha timu kuzunguka Mkoa mzima wa Mbeya hususani vijijini ili kutoa elimu na kuwatambua watoto wenye ulemavu ambao wanaishi majumbani na kushindwa kupatiwa misaada mbalimbali.


 
Hata hivyo amesema kuwa katika program hiyo pia itawawezesha wazazi, walezi, walimu  na viongozi wa Serikali kutambua namna ya kuwafundisha watoto wenye ulemavu kupitia elimu jumuishi kwa kumtambua mtoto kwa kumtofautisha kutokana na aina ya ulemavu alionao.

Awali mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homela aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune alitoa wito kwa jamii kuhakikisha wanasaidiana na wadau kufichua vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
 
Amesema tafiti zinaonesha kuwa ukatili dhidi ya watoto unafanywa na ndugu wa karibu hivyo kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kulinda haki za watoto kwa mujibu wa Katiba ya nchi kwa kutoa taarifa haraka ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kabla ya madhara hayajawa makubwa.
 
Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa viongozi wa dini waendelee kukemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwani madhara yake ni pamoja na kuongezeka kwa magonjwa ukiwemo Ukimwi, kuongezeka kwa watoto yatima, uzururaji, ombaomba na kutumikishwa katika kazi ngumu kinyume cha sheria ya Watoto ya mwaka 2009 kifungu cha 21.
 
Aidha Mfune amesema kuwa  kuwa ripoti ya Mwaka 2021 inaonesha kwa Mkoa wa Mbeya pekee watoto 1260 wamefanyiwa ukatili ambapo kati yao  wasichana ni  860 na wavulana ni 346 na kwamba kati ya hayo ukatili wa kingono ni watoto 244, kimwili 204, kihisia 492 na ukatili wa kiuchumi ni watoto 266.
 
Mfune amebainisha kuwa kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 watoto 114 ,2273 wanaishi katika mazingira hatarishi nchini huku watoto 4,8148 sawa na asilimia 42 pekee ndiyo wanaopata huduma na misaada mbalimbali.
 
Kwa upande wake Watoto walioshiriki maadhimisho hayo katika risala yao kwa mgeni rasmi iliyosomwa na Agatha Kisimba walitoa wito kwa wazazi na jamii kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakumba watoto.
 
Wamesema jamii ihakikishe watoto wanapata haki zao za msingi ikiwemo haki za kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kusikilizwa na haki ya kutoa maoni kama ilivyo kwa watu wengine bila kubaguliwa.