October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Yusuf Ngenya, (aliyevaa suti) akiangalia bidhaa mbalimbali za wazalishaji ambazo shirika hilo limezipatia vyeti na leseni ya kutumia alama ya ubora baada kuthibitishwa na kukidhi matakwa ya viwango. Hafla hiyo ilifanyika makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Wazalishaji wazidi kuchangamkia fursa TBS, wapatiwa leseni, vyeti

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuwakabidhi vyeti na leseni ya kutumia alama ya ubora ya shirika hilo wazalishaji ambao bidhaa zao zinathibitishwa na kukidhi matakwa ya ubora ikiwa ni moja ya mikakati ya kuhakikisha wanaondokana na vikwazo vya kibiashara.

Katika mwendelezo wa utaratibu huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wazalishaji 141 wakiwemo wakubwa, wakati na wadogo walikabidhiwa vyeti na leseni katika hafla iliyofanyika makao makuu ya shirika hilo yaliyopo Ubungo.

Kati ya wazalishaji hao 58 ni wazalishaji wadogo ambao wanazalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo vitakasa mikono, vyakula, vilainishi, vifaa vya umeme na vya ujenzi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi leseni hizo kwa wazalishaji hao, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Yusuf Ngeya, amesema imekuwa ni kawaida shirika kuwakabidhi vyeti na leseni za kutumia alama ya ubora wazalishaji ambao wanakidhi vigezo ili waendelee na uzalishaji wa bidhaa zenye ubora.

Amesema hatua ya bidhaa hizo kupatiwa vyeti na leseni ya kutumia alama ya ubora ya shirika hilo kutawafanya wazalishaji hao kuwa na uwezo wa kushindana na bidhaa nyingine sokoni, kuuza nchi za Afrika Mashariki bila bidhaa zao kulazimika kupimwa tena kwa ajili ya kuzithibitisha ubora na watapanua wigo wa biashara zao kwa kuyafikia masoko mengi zaidi.

“Ni wakati muafaka wa kuwapongeza na kuwapa moyo wajasiriamali wadogo ili nao waweze kuwa wakubwa kama wengine, tunakabidhi vyeti na leseni za ubora kwa wajasiriamali na kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu na hii ni kawaida yetu kila baada ya miezi mitatu kuwapongeza baada ya kupata vyeti vyao vya Ubora na leseni,”amesema na Dlt. Ngenya na kuongeza;

“Namshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa fursa kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bure pale wanapoomba bidhaa wanazozalisha wenyewe kuthibitishwe ubora na TBS.”

Dkt.Ngeya aliwataka wajasiriamali hao kuwa mabalozi wazuri wa TBS
kwa kuhamasisha wananchi wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda kuthibitisha ubora wa bidhaa zao wanazozalisha.

“Hakikisheni mnaendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika kila siku na sio leo mnapata leseni na cheti na badala yake mnaanza kutengeneza bidhaa zisizokuwa na ubora tutakuwa tunapita na kuwafanyia ukaguzi wa mara kwa mara, kwani sheria inaturuhusu kufanya hivyo,”amesema.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ihnemeter, ambayo inazalisha na kuuza vifaa vya umeme ikiwemo Meter, Abraham Rajakili, aliishukuru TBS kwa kuwapatia vyeti na leseni za ubora kwani huo ni mwaga mzuri wa kuingia sokoni kwa kukubalika zaidi na kujiamini.

“Kwa kweli tunawashukuru TBS kwa hatua hii tunaamini kuwa bidhaa zetu zitaweza kufanya vizuri zaidi sokoni kutokana na kuwa na nembo za ubora ya TBS,”amesema

Wakati huo huo, Dkt, Ngenya alisema kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu,TBS imesajili takribani majengo 513 ambayo yanashughulikia chakula na vipondozi na kusajili bidhaa ya chakula na vipodozi 596 kwa kipindi hicho.