Na Esther Macha ,Timesmajira,Online , Mbeya
WAZALISHAJI wa mbolea za asili na wakulima katika mikoa ya Mbeya na Songwe wameiomba serikali kutunga sera itakayohamasisha matumizi ya kilimo Ikolojia ambayo itahamasisha matumizi ya mbolea hiyo katika uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini na kusaidia kutunza mazingira.
Rai hiyo ilitolewa juzi na wakulima pamoja na wadau wanaohusika na uzalishaji wa mazao mbalimbali ambapo katika kikao hicho cha kujadiliana ni kwa namna gani kilimo cha Ikolojia kinaweza kuwasaidia wakulima kuzalisha kwa tija na kuongeza rutuba katika udongo, walisema utungaji wa sera unaweza kuwa msaada kuhamasisha kilimo hicho.
Miongoni mwa wakulima hao akiwamo Tujolege Mwakisunga anayejishughulisha na kilimo cha mpunga katika kijiji cha Ndobo wilayani Kyela alisema kuwa Serikali itengeneze mifumo mizuri ya kuboresha kilimo cha ikolojia ambacho kina tija kwa mkulima kutokana na kufanya majaribio katika msimu wa kilimo uliopita na kubaini kuongeza uzalishaji wa mazao mchanganyiko na kufufua ardhi iliyokufa kutokana na matumizi ya mbolea zenye sumu.
Mwakisunga amesema mfumuko wa pembejeo za kilimo umewaibua wabunifu wa kuzalisha mbolea ya asili ya kutumia samadi na mabaki mpunga hivyo ni wakati sasa Serikali kuwaunga mkono jitihada hizo ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuwepo masoko ya uhakika ya ndani na nje.
”Msimu huu wa kilimo tumepata shida sana bei ya pembejeo ilipata bei kupita kiasi tunashukuru wataalam wakiwamo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI kwa kushirikiana na Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA) walifanya utafiti wa udongo na kuhamasisha kilimo Ikolojia kinachohamasisha matumizi ya mbolea ya asili ili kuongeza uzalishaji wa mazao,” alisema Mwakisunga.
Amesema kilimo cha Ikolojia kupitia mashamba darasa ya mpunga walianzisha yameleta matumaini kwamba matumizi ya mbolea za asili yanaleta mavuno mengi na yenye ubora ukilinganisha matumizi ya mbolea za viwandani hivyo kutungwa kwa sera ya kuhamasisha matumizi ya mbolea asilia kwa kuzingatia kilimo Ikolojia ili kutunza mazingira kutaleta tija.
Ofisa Kilimo Kata ya Mababu Wilaya ya Kyela, Benjamin Mwaijumba, amesema kuwa uwepo wa kilimo cha Ikolojia kimekuwa na tija kwa wakulima kutokana na kuwepo kwa mfumuko wa gharama za pembejeo za kisasa.
“Tumepatiwa elimu kutoka kwa watafiti kutoka SUA na TARI, wakulima wameanza kunufaika na kilimo hicho kwa kuona mazao shambani yakichanua na kupendeza hali inayotajwa kurutubisha afya ya udongo ambayo imeharibiwa na matumizi ya mbolea za viwanda,” amesema Mwaijumba.
Mratibu wa Jukwaa la wadau wa kilimo wasio wa kiserikali nchini (ANSAF), Owen Nelson amesema kuwa utafiti waliofanya katika Sekta ya kilimo wamebaini uwepo wa manufaa makubwa kwa wakulima kutumia kilimo cha Ikolojia kwa kutumia mbolea ya asili tofauti na za kisasa.
Amesema wakulima wanapaswa kuzingatia elimu ya kitaalam katika uzalishaji pia serikali kuona umuhimu wa kuweka sera ya kuboresha kilimo cha ikolojia ili kuweza kutambulika ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa masoko kwa wazalishaji wa ndani.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba