November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawili washikiliwa kwa kukutwa na bastola bandia

Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online, Tanga

Jeshi la Polisi Mkoa Tanga linawashikilia watu wawili akiwemo Rodrick Masawe mkazi wa wilaya ya Muheza kwa tuhuma za kukutwa na Bastola (Pistol) Bandia iliyotengenezwa kienyeji akiitumia kufanyia vitendo vya uhalifu huku akijifanya kuwa ni mtumishi wa serikali wa jeshi la JWTZ.

Mtu mwingine anayeshikiliwa kwa tuhuma za kumiliki bastola iliyotengenezwa kienyeji ni Huruma John ambaye alikamatwa Mtaa wa Kisosora kata ya Nguvumali jijini Tanga.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga Henry Mwaibambe amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia silaha hizo kwenye matukio mbalimbali ya kihalifu.

Kamanda Mwaibambe amesema Rodrick Masawe alikamtwa katika kijiji cha Mamboleo Wilayani Muheza akiwa na Pistol Bandia na kujifanya mtumishi wa serikali wa jeshi la JWTZ ambapo mtuhimiwa huyo yupo mbaroni kwa hatua za kisheria.

Aidha Kamanda Mwaibambe ameelezea mtuhumiwa mwingine Huruma John aliyekamatwa na silaha ya Pistol bandia alikutwa eneo la Kisosora kata ya Nguvumali tarafa ya Chumbageni jijini Tanga akiwa na silaha hiyo kwenye begi lake la mgongoni ambapo mtuhimiwa anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Katika tukio jingine kamanda ameeleza kukamatwa kwa Mtua Wambura mwenye umri wa mika 50 mkazi wa mwakijembe kwa tuhuma za kukutwa na pembe tatu za mnyama aina ya Pongo akiwa amezihifadhi kwenye begi dogo nyumbani kwake kinyume cha sheria.

“Huko maeneo ya kijiji cha Songea kata ya Mwakijembe Wilayani Mkinga Mkoani Tanga alikamatwa Mtuwa Wambura mwenye umri wa miaka 50 kabila Mkamba kazi yake ni mkulima akiwa na pembe hizo uchunguzi unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika, “alisisitiza Kamanda Mwaibambe.

Hata hiyo kamanda ameeleza kuwa Mkoa wa Tanga umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kampeni ya usalimishaji wa silaha kwa hiari ambapo jumla ya silaha 488 zimesalimishwa.

“Mkoa wa Tanga umefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika usalimishaji wa silaha kwa hiari ambapo silaha zilizosalimishwa ni pamoja na Magobore 457, Shortgun 25, Rifle 3, na Pistal 3 hivyo jumla ya silaha 488 zimesalimishwa, “alibainisha Kamanda Mwaibambe.

Jeshi la polisi Mkoa wa Tanga limetoa wito kwa wananchi wote wanaozungukwa na miundombinu mbalimbali pamoja na hifadhi za wanyama pori kushirikiana na kulinda rasilimali hizo ili zilete manufaa kwa Taifa na pale watakabaini uharibifu au uhujumu wa wanyama pori watoe taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama au kwa viongozi wa serikali walio karibu nao.