Na Angela Mazula,TimesMajira Online
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa wawekezaji kutoka nje ya nchi itawachukua siku saba tu kupata vibali vyote kutoka siku `14 zilizokuwa zimependekezwa na Rais John Magufuli.
Pia amewataka wawekezaji wa ndani ya nchi kuwafichua warasimu na wala rushwa kutoka taasisi za umma zenye jukumu la kuwasaidia katika uwekezaji.
Majaliwa amesema hayo katika uzinduzi wa maonesho ya tano ya bidhaa za viwanda Tanzania yanayoendelea katika Viwanja vya Maonyesho jijini Dar es Salaam ambapo amesema serikali licha ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani pia inazidi kuweka mazingira bora ya wawekezaji wa nje ya nchi.
Aidha, amesema kwa kuhakikisha azima hiyo inatimia imenuia kutoa vibali kwa wawekezaji ndani ya siku saba ikiwa ni pamoja na kukabiliana na kila aina ya urasimu ambao umekuwa unakwamisha uwekezaji.
Akizungumzia kuhusiana na kusaidia wawekezaji wa ndani ya nchi Majaliwa amewataka kukabiliana na urasimu kwa kufichua wanaowaomba rushwa na kuwapuuza wale ambao wamekuwa vikwazo katika kufanikisha uwekezaji wao.
‘’Serikali inatambua nguvu ya kusaidia ukuaji wa uchumi kutoka kwa wawekezaji wa ndani na kamwe haiwezi kuwaacha,’’amesema.
Amesema, Serikali kwa kutambua hilo imekuwa ikiwakutanisha mara kwa mara wafanyabiashara na mamlaka zenye jukumu la kuinua biashara na uwekezaji nchini ili kuweza kupata fursa ya kusikilizwa na kutatuliwa kero za biashara zao.
Amesema Tanzania inaweza kufanya biashara kubwa na nchi za Malawi, Zambia, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo lakini kumekuwa na changamoto kadhaa zinazokwamisha biashara kutokuwa kubwa kama inavyotakiwa.
Amesema, katika kuhakikisha wafanyabiashara wa hapa nchini wananufaika na fursa za kibiashara Serikali imeanzisha utoaji wa mikopo kupitia taasisi zake za fedha na kuwataka wafanyabiashara kukopa kwenye taasisi hizo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amebainisha kuwa ipo mifuko kadhaa inayotoa misaada ya kiteknolojia kwa wawekezaji wa ndani ya nchi ili kuwawezesha kukabiliana na ushindani wa kibiashara.
Waziri MKuu pia ameagiza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kuwawezesha wawekezaji wa ndani kuuza bidhaa zao siku zote katika viwanja hivyo vya sabasaba ambapo maonesho hayo yanaendelea.
“Huu ni mwaka wa tano yanafanyika maonesho haya, hii ni hatua kubwa katika kuinua uwekezaji nchini na niwahakikishie kuwa Serikali imelenga kuwainua wafanyabiashara wa ndani kama ilivyo kwa wale wa nje.
Mazingira ya ufanyaji biashara yanazidi kuboreshwa zaidi na zaidi na kama mnavyokumbuka Rais Magufuli wakati akizindua bunge alipinga urasimu kwenye uwekezaji sasa ninaambiwa kuwa siku za kutoa vibali zitakuwa saba tu na haya ni mafanikio,”amefafanua.
Amewataka kutanua wigo wa biashara zao kwa kubadilisha mitandao ya kazi na kupanua wigo wa biashara zaidi.
Majaliwa ametolea mfano wa ubunifu wa kutwanga mpunga alioukuta katika banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na kusisitiza kuwa ubunifu kama huo ni lazima kuendelezwa huku akiwataka wadau wengine kwenda kuungana nao katika kuhakikisha ubunifu huo unawafikia wakulima.
More Stories
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua