December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wavuvi wadogo wampa maua yake Rais Samia

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wavuvi wadogo hapa nchini wamejinasibu kutembea kifua mbele kwa sababu ya mipango mizuri ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoiweka juu ya kuwasaidia wavuvi kuinuka na kuboresha shughuli zao.

Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa wavuvi wadogo hapa nchini, Feisal Mohamed Ali wakati akitoa salamu kwenye Mkutano wa Wavuvi Wadogo Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 5-7,2024.

“Hivi sasa tunatembea kifua mbele kwa sababu tunaona vitendo vinavyofanywa na mhe. rais, tunaona ugawaji wa boti, utoaji wa mikopo ya riba nafuu kwa wavuvi, lakini kubwa zaidi ni ujenzi wa bandari ya uvuvi ya kilwa masoko ambao ndio unakwenda kuwa muarobaini wa kuleta mabadiliko ya sekta ya uvuvi hapa nchini”, alisema

Aliongeza kwa kusema kuwa jitihada zote hizo zinazofanywa na Rais Samia ni ishara ya nia yake thabiti ya kutaka kumuinua mvuvi hapa nchini.

Alifafanua kwa kusema kuwa nia njema ya rais Samia ya kutaka kumuinua mvuvi inajidhirisha pia katika kiasi cha bajeti anachokitenga kwa ajili ya wizara ya mifugo na uvuvi ambayo imekuwa ikipanda kuanzia mwaka 2021 kutoka bilioni 73 mpaka kufikia bilioni 330 mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 600 kwa muda wa miaka 3.

Alibainisha kuwa kufuatia dhamira njema hiyo aliyonayo rais samia kwa wavuvi, ahadi yao kwake ni kuendelea kumuunga mkono yeye pamoja na hawata muangusha.