December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wavamizi Msitu wa Kuni wampongeza Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Morogoro

UAMUZI wa Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia ekari 5,113 za ardhi wakazi wa eneo la Msitu wa Kuni maarufu CCT, Kata ya Dakawa wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro umepongezwa na wananchi wakisema hicho ni kielelezo cha jinsi Rais huyo alivyodhamiria kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Wakizungumza na Majira mkoani Morogoro jana, wananchi hao walisema walipokea kwa mikono miwili uamuzi huo wa Rais Samia, kwani kwa muda mrefu walishindwa kufanya shughuli zao maendeleo kutokana na kuwepo mgogoro huo.

Mmoja wa wakazi hao, Jonesiah Paul alisema mgogoro huo ulikuwa ukihatarisha usalama wao, hivyo kitendo cha Rais Samia kuamua kuhitimisha mgogoro huo unastahili kupongezwa.

Uamuzi huo ulitangazwa jana na kamati ya mawaziri nane wa kisekta kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika eneo hilo.

“Kimsingi, Rais ameamua kutubakiza hapa kwa huruma yake, watu walivamia eneo la hifadhi ambalo ni hifadhi ya Msitu wa Kuni, lakini alichokisema Rais Samia hi huruma, hakuna mtu ambaye alistahili kuwepo hapa,” alisema Paul.

Naye Evance Johansen, alisema kitendo cha wananchi wavamizi kupewa eneo la ardhi lenye ukubwa wa hekari 5,113 ni kielelezo kwamba Rais Samia ni mtu wa watu.Kwa mujibu wa kamati hiyo inayoongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, wakazi hao awali walivamia eneo hilo ambalo ni hifadhi ya Msitu wa Kuni.

“Tumheshimu mheshimiwa Rais kwa huruma yake hii ya kuwapa eneo kwa sababu nyinyi ni wavamizi wa Msitu wa Kuni na mlitakiwa kutoka wote, ila amewapa ekari 5,113 ili muweze kujenga makazi yenu,” alisema Ndaki.

Eneo hilo la hifadhi limekuwa na mgogoro wa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 20 na wananchi wamekuwa wakivamia kwa nyakati tofauti na kujenga majengo ya kudumu.

Novemba 30 mwaka huu, Serikali ya Wilaya ya Mvomero kwa kushirikiana na idara ya ardhi ilianza kazi ya ubomoaji wa nyumba katika eneo hilo na wananchi zaidi ya 30 walivunjiwa nyumba na kukosa mahali pa kuishi.

Awali katika ubomoaji huo, Mkuu wa wilaya hiyo, Halima Okashi akizungumza na wananchi hao aliwataka kufuata sheria huku akieleza nyumba zote zilizojengwa baada ya uhakiki zitabomolewa na Serikali, kwani ilitoa nafasi ya kuwataka wazibomoe wenyewe lakini hawakutekeleza agizo hilo, hivyo sheria inafuata mkondo wake.

Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Morogoro, Frank Mizikuntwe alisema Serikali ilitoa maelekezo halali ya kusimamisha ujenzi na kukiuka, ndio maana nyumba zilizohakikiwa hazikuguswa.

Katika ziara ya mawaziri hao juzi, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete alimtaka Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro, Mizikuntwe kuwapanga wakazi hao katika eneo lililoruhusiwa ndani ya siku 90.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja aliwataka wananchi waliovamia eneo ambalo halipo katika yale aliyoyatoa Rais waondoke mara moja na kuwataka kutoendelea na ujenzi, ili kuepuka kubomolewa makazi yao.

Wakazi wa eneo hilo walipokea kwa mikono miwili agizo hilo la Rais na kumshukuru kwa kuwagawia eneo hilo, ili waendelee na ujenzi katika eneo lililoruhusiwa.

Mkuu wa Mkoa Morogoro, Fatuma Mwasa hivi karibuni baada ya kutokea kwa bomoabomoa hiyo alieleza eneo lililotolewa na Rais Samia ni kwa wale waliohakikiwa na wengine wataondolewa katika Milima ya Uluguru kwa ajili ya kupisha vyanzo vya maji.