January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wauguzi,Wakunga kada yenye thamani katika kupunguza vifo vya uzazi

Na Catherine Sungura,TimesMajira online

MCHANGO wa kada ya Uuguzi na Ukunga Tanzania ni mkubwa, watumishi wa kada hizi hufanya kazi saa 24 siku saba za wiki, wakitoa huduma kwa wananchi, kwa zaidi ya asilimia 80 ya huduma zote za afya.

“Serikali inatambua umuhimu wa kada hizi nchini katika maendeleo ya sekta ya afya,” ni kauli yake Waziri wa Afya,Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima.

Februari,mwaka huu Jijini Dodoma,Dkt.Gwajima alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa wauguzi viongozi, ukiwa na kauli mbiu isemayo “Huduma Bora Inayojali Utu,Heshima, Upendo na Maadili…Ni Haki ya Kila Mwananchi”:Malalamiko Sasa Basi.

“Ni wazi kuwa Wauguzi na Wakunga ni raslimali kubwa na nguvu kazi kubwa katika sekta ya afya nchini na duniani kote.Ni watoa huduma ya afya ambao wako mstari wa mbele katika kutoa huduma wakati wote kwa kuwahudumia wagonjwa (wateja) wenye uhitaji bila kuchoka,” anasema.

Anaongeza ”Ni Dhahiri kwamba, kwa umoja wao na kwa kutumia taaluma, ujuzi na weledi wao wanaweza wakatoa majibu ya kwa nini huduma kwa wateja katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini zinakuwa na changamoto kiasi cha kuleta malalamiko kwa baadhi ya wateja.

“Wauguzi,Wakunga na watoa huduma wengine wote katika sekta hii wanapaswa kutoa huduma zinazozingatia Utu, Heshima,na Upendo kwa wagonjwa (wateja).

“Wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwajali na kuwatunza wagonjwa na kuwahudumia kwa utaalam,weledi, ubunifu na mtazamo chanya kwa kufuata maadili ya taaluma zao na Miongozo hii,” anasisitiza Dkt. Gwajima.

Anasema hatua hiyo itaimarisha huduma na kuwavutia wananchi kutumia zaidi huduma za afya hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye mpango wa bima kwa wote.

THAMANI YA HADHI YAO

Anaongeza “Nchi yetu, Wauguzi na Wakunga ni zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi katika sekta ya afya, wana mchango mkubwa katika utekelezaji wa Malengo ya Afya hasa upatikanaji wa Afya ya msingi (Primary Health Care) katika jamii yetu ambako zaidi ya watanzania asilimia 75 wanapatikana.

“Afya hii ya msingi ni nguzo kubwa katika kujenga Taifa lenye afya na ustawi mzuri katika maendeleo ya uchumi hususani wakati huu ambapo Tanzania imefikia uchumi wa kati,” anasema.

Anasema kada hiyo ina dhamana kubwa katika kuleta matokeo makubwa katika sekta hiyo nchini, Serikali iliona umuhimu huo na kwamba mwaka wa fedha 2015/16 ilipandisha hadhi Kitengo cha Huduma za Uuguzi na Ukunga na kuwa Idara kamili.

“Hii ni baada ya kuona mchango wao mkubwa katika kutoa na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo yote nchini.

“Aidha, viongozi túnalo jukumu kubwa la kubuni, kusimamia na kuweka malengo na mikakati endelevu ya kuinua utoaji huduma za afya katika maeneo yetu ya kazi,” anasisitiza.

Dkt.Gwajima anaongeza “Nimefurahishwa na hatua zinazochukuliwa na idara hii katika kuimarisha usimamizi wa huduma za kada hizi nchini.

“Ikiwemo utengenezaji wa miongozo mbalimbali ya kusimamia huduma za Uuguzi na Ukunga kama vile Mwongozo wa Huduma inayojali Utu, Heshima na Upendo (Respectful and Compassionate Care).

“Mwongozo huu ukitekelezwa kikamilifu basi tutapunguza malalamiko mengi toka kwa wananchi na hatimaye watavutiwa kuja kupata huduma katika vituo vyetu,” anasema.

Anawapongeza kwa kuanzisha na kusimamia mpango wa NIMART (Nurse Initiated Management of Anti-retroviral Theraphy) ambao unachangia katika kupambana na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI nchini.

“Mpango huu unachangia kuongeza upatikanaji wa huduma ya dawa za kufubaza maambukizi ya VVU kwani sasa mpaka zahanati zinafungua CTC clinic zinazohudumiwa na Wauguzi waliopata mafunzo haya,” anasema.

Anasema wataalamu wa kada hizo wamesaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI ikiwemo kuanzisha dawa za kufubaza makali ya VVU kutoka alisimia 39 Mwaka 2017 hadi Asilimia 84 mwaka 2020 na upimaji wa VVU kutoka Asilimia 72 Mwaka 2017 hadi asilimia 96 Mwaka 2020.

“Hii imesaidia nchi yetu katika jitihada za kufikia malengo ya Kimataifa ya 90-90-90, ni vyema kuongeza kasi zaidi na niwaombe wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na idara ya hii ili tuweze kupata matokeo makubwa zaidi,” anabainisha.

Anasema Serikali ya ipo katika mkakati mahususi wa kuboresha huduma za afya nchini ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi,vifo vya watoto wachanga na watoto walio chini ya miaka mitano.

“Shirika la Afya Duniani (WHO) na Serikali yetu inatambua kada hizi mnaweza kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 80 wakitekeleza kikamilifu majukumu yao wakizingatia afua mbalimbali zinazohusu afya ya uzazi na mtoto.

“Katika kutambua na kuhakikisha,vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga na watoto walio chini ya miaka mitano vinapungua au kuondoka kabisa Serikali imeamua kulitekeleza kwa vitendo kwa kuongeza bajeti ya sekta ya afya kutoka Sh.bilioni 796.11 mwaka 2015/16 na kufikia Sh.bilioni 933.28 mwaka 2020/2021,” anasema.

Anafafanua “Lengo la hatua hii ni kusaidia na kurahisisha uendeshaji wa sekta ya afya na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.Pia Serikali imeongeza kiasi cha pesa kinachotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na chanjo kutoka Sh.bilioni 31 mwaka 2015/16 na kufikia Sh.bilioni 246 mwaka 2020/2021.

“Serikali inaendeleza juhudi za kuinua uchumi wa nchi kwa kuongeza idadi ya viwanda ikiwa ni pamoja na viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba hapa nchini ili kuongeza upatikanaji wa huduma.

“Pia imechukua hatua mahsusi za kuimarisha huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga na watoto wa umri chini ya miaka mitano.

“Tulijitahidi wakati wa utekelezaji wa malengo ya milenia kupunguza vifo hivi,japo takwimu za hivi karibuni zimeonesha kutoridhisha kuongezeka kwa vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua kutoka 432 (TDHS 2010) hadi 556 (2015) kati ya vizazi hai 100,000,” anatoa rai.

Dk.Gwajima anaongeza “Kwa upande wetu serikali tutaendelea na jitihada za kuboresha huduma ya afya ya uzazi na mtoto ikiwemo huduma ya msingi ya dharura na za upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.

AJIRA NA MAADILI

“Serikali imeendelea na itaendelea kuajiri na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wakiwemo wa kada hizi wenye weledi na kuwapanga katika maeneo yenye upungufu mkubwa ili kuhakikisha wanachi wote wanapata huduma kwa usawa na kwa wakati,”anasisitiza Waziri huyo mwenye dhamana ya masuala ya afya nchini.

Pamoja na hayo,anasisitiza maadili ya mtumishi wa umma bila kujali iwapo ni kiongozi au la,ni viwango vya uadilifu vinavyotazamiwa na wananchi kwa watumishi wote wa umma.

“Maadili huwekwa kwa njia ya misingi,kanuni na miongozo inayotakiwa katika utumishi na wananchi hutumia kupimwa mwenendo wa kila mtumishi wa umma,” anasema.

Anaongeza“ Kanuni na Misingi hiyo huwekwa kwa kuzingatia utu,dhamira safi, maslahi ya walio wengi,ubora na utamaduni wao.Maadili huzuia matumizi mabaya ya madaraka au dhamana.Kwa hiyo,maadili hutumika kupima ubora wa huduma au dhamana iliyotolewa na waliokabidhiwa.

“Chimbuko la Maadili ya Utumishi wa Umma hapa kwetu Tanzania yametajwa katika Nyaraka za Serikali kama vile, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977; Sera ya Menejimenti ya Ajira, ya mwaka 1999; Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002; na Kanuni za Utumishi wa Umma, za mwaka 2003 (Public Service Regulation Act).

“Ili Mtumishi wa Umma awe mwenye ufanisi na wa kuheshimika, anapaswa kuzifuata Kanuni za Maadili ya Utumishi kwa kuzingatia mambo yafuatayo: Kutoa huduma bora, utii kwa Serikali; bidii ya Kazi; na kutoa huduma bila upendeleo.Vilevile anatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu; kuwajibika kwa Umma; kuheshimu Sheria; na Matumizi sahihi ya Taarifa.

“Lakini pamoja na kuwepo kwa nyaraka zote hizi bado watumishi wameendelea kufanya kazi kinyume na matakwa ya taaluma zao,” anasisitiza.

Anaongeza “Mara nyingi tumepokea malalamiko juu ya ucheleweshaji wa utoaji huduma,upendeleo,mienendo mibaya ya watumishi,ubinafsi katika kazi; rushwa, vitendo vya Jinai (Wizi) na matumizi mabaya ya madaraka.

“Ni jukumu letu sisi kama viongozi kusimamia watumishi walioko chini yetu ili waweze kutoa huduma kwa wateja kwa kuzingatia maadili katika utumishi wa umma na kuepukana na matendo haya yaliyotajwa hapo juu.

“Niagize mabaraza na vyama vya kitaaluma kuendelea kukemea na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wanaokwenda kinyume na maadili ya taaluma zao,” anatoa agizo.

Anasisitiza Serikali na Wizara anayoisimamia itaendelea kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo kupitia upya kwa miundo ya maendeleo ya watumishi katika sekta ya afya.

“Kuhakikisha upatikaji wa Vifaa tiba na dawa ili wananchi wapate huduma bora za afya. Kubuni mikakati mbalimbali ili kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi,vifo vya watoto wachanga na wenye umri chini ya miaka mitano, kuangalia upya Muundo wa uongozi katika Sekta ya Afya ili uweze kuwa jumuishi na Kada zingine,” anasema.

Anaongeza ”Naomba wauguzi na wakunga tuendelee kujiendeleza ili tupate wauguzi bingwa zaidi watusaidie kuimarisha upatikaji wa huduma za kibingwa katika hospitali zetu nchini, vile vile idara hii iongeze kasi zaidi ya kusimamia ili kuboresha upatikanaji wa huduma bora za Uuguzi na Ukunga nchini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitenga mwaka 2020 kuwa mwaka wa Wauguzi na Wakunga duniani na kuadhimishwa duniani kote kama njia ya kuenzi mchango muhimu unaotolewa na Wauguzi na Wakunga duniani kote katika kuleta mapinduzi makubwa katika Huduma za Afya.

Mkutano huo wa viongozi wa kada hiyo ya uuguzi na ukunga umefanyika nchini ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha maadhimisho hayo