September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wa Mungu wanaopotosha jamii waonywa

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

WATUMISHI wa Mungu ambao wamekuwa wakipotosha waumini na kuwahadaa kuwa wakitumia maji na mafuta watapata mahitaji yao yote na kuwa matajiri wameonywa na kutakiwa kuacha tabia hiyo mara moja.

Onyo hilo limetolewa juzi na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Ramadhan Kapela kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba, alipokuwa akizungumza na waumini wa kanisa la TAG Maranatha Cheyo kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.

Amesema kuwa hakuna mtu anayeweza kupata utajiri pasipo kufanya kazi, huo ni uongo, hivyo akasisitiza kuwa Watumishi wa Mungu wanaohadaa waumini kuwa wakitumia maji na mafuta au vitu vinginevyo watapata utajiri hao ni matapeli.

Kapela amebainisha kuwa serikali inaheshimu imani ya kila mtu na inaunga mkono kazi nzuri zinazofanywa na Viongozi wa dini lakini haikubaliani na watumishi wanaotembea na vibegi vyenye mafuta na maji na kudanganya watu.

Amesema kuwa serikali ya awamu ya 6 imekuwa ikisisitiza kila mtu kufanya kazi ili kujipatia kipato ila watumishi wanaodanganya wananchi kununua mafuta, maji au vitu vinginevyo ili wawe matajiri hao hawana utofauti na waganga wa kienyeji.

‘Serikali haina dini, kila mtu anaruhusiwa kuabudu dini anayotaka, ila kuweni makini na watumishi wanaowahadaa, fanyeni kazi na Mungu atabariki kazi za mikono yenu na mtapata mafanikio makubwa’, amesema Mstahiki Meya.

Mstahiki Meya ameongeza kuwa serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kwa ukaribu zaidi na Viongozi wa Dini, inaunga mkono na inathamini mchango wao katika kudumisha amani na utulivu wa nchi.

Naye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo Rev.Lutengano Mwasongela amesema kuwa kanisa hilo linaunga mkono juhudi zote zinazoendelea kufanywa na serikali ili kuwaletea maendeleo wananchi ikiwemo kushirikiana na madhehebu ya dini.

Ameomba serikali kuendelea kuchukua hatua stahiki kwa wale wote watakaobainika kuchafua taswira ya nchi ikiwemo kujihusisha na vitendo vya utekaji au mauaji ya watu wasio na hatia ili kukomesha vitendo hivyo.

Aidha kuelekea kwenye uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa, ametoa wito kwa waumini wa kanisa hilo na makanisa mengine kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na wale watakaopenda kugombea wajitokeze kuwania nafasi hizo.