Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Patrobas Katambi,amewataka watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuzingati wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu kabla ya kudai haki zao.
Katambi,amesema hayo jijini hapa,leo Disemba 12,2023 alipokuwa akifungua mkutano wa baraza kuu la 53 la wafanyakazi wa shirika hilo unaofanyika kwa siku mbili kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji.
Amesema TANESCO imekuwa ikishambuliwa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na umeme kukatika baadhi ya maeneo,hivyo amesema ili kuepukana na hayo ni kuzingatia wajibu wao ili wananchi wapate umeme kama wanavyostahili.
“Kabla ya kudai haki zetu lazima tuangalie wajibu wetu katika maeneo yetu tumeyatimiza kwa ukamilifu kwani suala la umeme nchini ni jambo la muhimu sana hivyo tunapaswa kutimiza majukumu yetu ili kuondoa malalamiko ya mgao wa umeme nchini,”amesema
Vilevile amelitaka Shirika la hilo kuzingatia maslahi ya watumishi wake ili kuongeza ufanisi na ubunifu katika kutekeleza majukumu yao.
Katambi amesema ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa watumishi ndani ya shirika hilo maslahi yao yanapaswa kupewa kipaumbele ili kuongeza uwajibikaji.
“Ili kuongeza ufanisi wa shirika letu hili ambalo tunalitegemea katika uzalishaji wa umeme mnapaswa kuzingatia maslahi ya watumishi wenu kwa kuwapa motisha, posho, kupandishwa vyeo ili kuwaondolea stres watumishi na kuongeza tija an ubunifu katika shirika hili tunalolitegemea kwa kuzalisha nishati ya umeme nchini,”amesema Katambi
Hata hivyo amewataka watumishi wa TANESCO kupuuza maneno wanayotupiwa kwenye mitandao kwani mengi yanakuwa hayana uhakika na badala yake wafanye kazi kwa bidii na kuelimisha wananchi ili kuondokana na maneno ya kwenye mitandao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Gissima Nyamo-hanga ametaja lengo la Mkutano huo kuwa ni kujadilia mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya kiutendaji.
Nyamo-hanga amesema kuwa mkutano huo unawapa fursa watumishi kuchangia mawazo yao na jinsi ya kuyafanyia kazi ili kuboresha huduma zao kwa wananchi.
Pia amesema maagizo yote yalitolewa na Naibu waziri Katambi watayafanyia kazi ili kuongeza ufasi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwa watumishi wao.
“Baraza kuu la wafanyakazi ni chombo ambacho pia majukumu yake ni kuangalia maslahi na haki za wafanyakzi hivyo pia katika kikao chetu tutakwenda kujadili masuala ya maslahi kwa watumishi na haki zao,”amesema.
Pamoja na hayo amezungumzia hali ya upatikanaji wa umeme nchini baada ya kuulizwa swali na mwandishi wa habari kuhusu mvua zinazonyesha zinachangia kwa kiasi gani upatikanaji wa umeme nchini ambapo amesema mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini hasa kanda za Pwani zimeongeza uzalishaji katika vyanzo vilivyopo nchini.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi