November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi Madini waendelezwa kuboreha utendaji

Na Nuru Mwasampeta,WM

IMEELEZWA kwamba Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imepeleka watumishi 45 masomoni na miongoni mwao watumishi 15 wanasomeshwa kozi za muda mrefu na 30 wanasoma kozi za muda mfupi ili kuwajengea uwezo na kuboresha utendaji wao.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Madini, Issa Nchasi alipokuwa katika mahojiano ya moja kwa moja katika kipindi cha Baragumu kinachorushwa mubashara na Channel Ten jijini Dar es Salaam.

Ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoadhimishwa kila mwaka kuznzia Juni 16 hadi 25 kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo Tanzania inaadhimisha wiki hiyo kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni, 2021.

Akijibu swali kutoka kwa watangazaji juu ya matamanio yake kwa watumishi wa Wizara ya Madini, Nchasi amesema, katika mambo ya kiutumishi kuna suala la haki na wajibu na kubainisha kuwa wizara inahakikisha watumishi walionao wanaendelezwa, lakini pia wanapata vitendea kazi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi na baadaye kufuatilia je? Mtumishi amewajibika katika majukumu yake ipasavyo.

Pamoja na hayo, Nchasi amewaalika wadau wa madini wa ndani na nje kufika katika banda la maonesho lililopo katika ofisi ndogo za wizara mjini Dodoma katika jengo la GST ili kupata ufafanuzi na elimu kutoka kwa wataalamu wao waliopo katika banda hilo.

Amesema, maoni na malalamiko yote yanayowasilishwa na wadau katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yatafanyiwa kazi na kuhakikisha kero zote zilizowasilishwa zinatatuliwa.

Akizungumzia masuala mengine yanayohusu Sekta ya Madini Nchasi amesema, suala la uongezaji thamani madini linatiliwa mkazo sana na wizara yake na hivyo kukisimamia kwa nguvu Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kilichopo jijini Arusha kinachotoa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito.

Ameongeza kuwa, uzinduzi wa kiwanda cha mwanza Precious Refinery kilichozinduliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan mchakato wa ujenzi wake ulilenga katika kuhakikisha madini yanayochimbwa nchini yanasafirishwa yakiwa yameongezewa thamani na hivyo kuuzwa kwa bei nzuri tofauti na yakiuzwa yakiwa bado ni ghafi.

Amesema, suala la uongezaji thamani linatiliwa mkazo ili wananchi wapate ajira na kuuza madini kwa bei nzuri ili kuongeza kipato.

Akizungumzia suala la teknolojia Nchasi amesema, wizara imelipa kipaumbele kwa kiasi kikubwa na kubainisha kuwa wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa limejenga viwanda vitatu vya kuwasaidia wachimbaji wadogo ili waweze kupata elimu ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini kwa tija zaidi alisema viwanda hivyo vimejengwa katika Mkoa wa Geita na Mkoa wa Mbeya.

“Wachimbaji wamepewa fursa ya kwenda katika viwanda hivyo kupata mafunzo na huduma za kuchenjua madini ya dhahabu kwa gharama nafuu,”Nchasi amebainisha.

Akijibu swali la kwanza la mtazamaji aliyehoji kuhusu utolewaji wa leseni kufanyika mwezi Julai, pekee kwa kila mwaka, Nchasi amesema mwombaji yeyote wa leseni ya uchimbaji mdogo wa madini atapata majibu ya maombi yake wakati wowote kwa kuwatumia maafisa madini wakazi waliopo katika mikoa yao na kubainisha kuwa kila mkoa una ofisi hizo za madini.

Aidha, Nchasi akijibu swali jingine lililoulizwa na mtazamaji kuhusu suala la upandishwaji wa madaraja amesema jambo hilo haliji tu isipokuwa linafuata taratibu zote za kiutumishi zilizowekwa ikiwa ni pamoja na muda wa mtumishi katika cheo husika pamoja na utendaji wake na kuwataka watumishi wanaolalamikia kutokupandishwa vyeo kuwafikia waajiri wao ili kuelezwa sababu hasa ya kutopandishwa cheo.

Akielezea kuhusu ‘branding’ ya madini ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee, Nchasi alisema kwa sasa suala la utoroshaji wa madini hayo limepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na uanzishwaji wa masoko ya madini kwani usimamizi wake ni wa uhakika.

Aidha, ameongeza kuwa, wizara inafanya taratibu kuhakikisha popote madini hayo yatakapopatikana yatakuwa na alama inayoonesha kuwa yametoka Tanzania.

Akifafanua kuhusu mtumishi wa umma, Nchasi alimtaja mtumishi wa umma kuwa ni yule anayehudumu katika ofisi za umma zikiwepo wizara, taasisi za serikali na mashirika na mamlaka mbalimbali ya umma.

Amesema wiki hii inawataka watumishi wa umma kujitafakari wametoka wapi, wapo wapi na wanakwenda wapi katika kutumikia umma aidha, kuona namna ya kutatua changamoto mbalimbali za kiutumishi na jamii wanayoihudumia.

Nchasi alieleza kwamba, chimbuko la Madhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni mwaka 1994 nchini Morocco ambapo mawaziri wenye dhamana na utumishi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika waliazimia kuanzisha suala zima la kuwatambua watumishi wa umma.

Alibainisha kuwa, watumishi waliokuwa wakihudumia serikali ya kikoloni katika taifa lolote lililotawaliwa Afrika walikuwa wakikidhi matakwa ya wakoloni katika kuhakikisha rasilimali zinapatikana kwa ajili ya kutumika na kusafirishwa katika nchi zao, hivyo baada ya uhuru ikaonekana miongozo iliyopokelewa kutoka kwa wakoloni haikuendana na nia na madhumuni ya nchi za Afrika baada ya kupata uhuru kutokana na mapungufu hayo mataifa yanayounda Umoja wa Afrika yakaamua kurekebisha ili sekta za utumishi wa umma ziweze kutimiza matakwa ya serikali na wananchi wa mataifa hayo.

Hivyo kufuatia maono hayo nchi wanachama wakaamua kuanzisha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ili kutambua changamoto za watumishi pamoja na wadau wa sekta mbalimbali za umma na baadaye kutatua changamoto hizo na kutoa huduma kwa mujibu wa taratibu na miongozo mbalimbali ya kiutumishi.

Akielezea mafanikio ya Tanzania tangu kuanzishwa kwa wiki ya utumishi wa umma, Nchasi alisema, kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwepo kuanzishwa kwa Mkataba wa Huduma kwa Mteja unaomtaka mtumishi kutekeleza jukumu fulani kwa muda na viwango sahihi vilivyobainishwa katika miongozo mbalimbali ya kiutumishi.

Akizungumzia mashirikiano ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika zinazoadhimisha wiki hii alisema kwa kuangalia kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inaonesha wazi kwamba Waafrika wote tunalenga katika kuhakikisha tunatumikia umma kwa uadilifiu.

Kufuatia kauli mbiu ya maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma inadhihirika kuwa nchi huru za Afrika zina mipango ya pamoja katika utekelezaji wa majukumu yake huku ukiwekwa mkazo mkubwa katika suala la uadilifu.

Amesema,kauli mbiu kuu ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa Mwaka 2021 ni “ Kujenga Afrika Tunayoitaka, kupitia utamaduni wa Uadilifu ambao unastawisha uongozi wenye maono hata katika mazingira ya migogoro” na hii inaonesha ushiriki wa wizara taasisi zilizochini ya wizana na nchi katika katika kuadhimisha wiki hii inayoadhishwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika.