December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi kukaimu nafasi muda mrefu ni kikwazo

Na James Mwanamyoto,TimesMajira Online,Morogoro

TATIZO la watumishi wa umma kukaimu nafasi za uongozi kwa muda mrefu bila kupata stahili ya vyeo wanavyokaimishwa, linatokana na waajiri kutozingatia taratibu za kiutumishi pindi wanapowakaimisha watumishi hao kama Waraka wa Utumishi Namba 2 wa Mwaka 2018 unavyoelekeza.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mst), George Mkuchika

Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mst), George Mkuchika alipoitembelea Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Waziri Mkuchika amesema, kumekuwa na tabia ya waajiri wengi hususan katika halmashauri kuwakaimisha watumishi ambao hawana sifa za kukaimu wala kibali cha kukaimu ambacho kinatolewa na Katibu Mkuu-Utumishi

Amefafanua kuwa,ili mtumishi aweze kukaimu,anapaswa kuwa na cheo cha Afisa Mwandamizi na kuendelea na pia awe amepatiwa kibali cha kukaimu nafasi husika na Katibu Mkuu- UTUMISHI ambacho atakitumikia kwa miezi isiyozidi sita kabla ya kuthibitishwa rasmi iwapo atakidhi vigezo vya kukitumikia cheo hicho.

Waziri Mkuchika ameongeza kuwa, kitendo cha watumishi kukaimishwa bila kufuata taratibu kimekuwa ni chanzo cha malalamiko ya watumishi wengi, hivyo aliwataka waajiri kuzingatia taratibu ili kuepuka malalamiko ambayo yanashusha morali ya utendaji kazi.

Wakati huo huo,Waziri Mkuchika amewataka waajiri kuhakikisha wanawawezesha wastaafu kupata mafao yao kwa wakati pindi wanapostaafu ili kuwaondolea usumbufu wa kufuatilia mafao yao pindi wanapostaafu ikizingaatiwa kuwa wamelitumikia taifa kwa bidii na uadilifu.

Mkuchika amesema, ili wastaafu wapate mafao kwa wakati,maafisa utumishi wanapaswa kufanya maandalizi kwa kukusanya vielelezo vyote vinavyohitajika mapema miezi sita kabla.

“Kutokana na changamoto hii, nitafanya mkutano na maafisa utumishi nchi nzima kama nilivyoahidi hapo awali ili kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu suala hili,”amesisitiza Waziri Mkuchika.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekekezaji ya Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhandisi Emmanuel Kalobelo amemweleza Waziri kuwa, pamoja na mafanikio mazuri yaliyopatikana katika Mkoa wa Morogoro, ofisi yake ina changamoto ya watumishi kukaimu kwa muda mrefu na wastaafu kutokapata mafao yao kwa wakati pindi wanapostaafu.