Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Ileje.
KATIBU Tawala (RAS) wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Nuru Kindamba na timu ya uendeshaji ya Halmashauri (CMT) kujitathmini kuhusu utendaji kazi wao.
Huku akiiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha kiasi cha shilingi milioni 80.2 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati mbili katika vijiji vya Shinji na Mtima katika kata ya Mbebe, Wilayani humo.
Seneda ametoa maelekezo hayo, Disemba 5, 2023 baada ya kufanya ziara katika vijiji hivyo na kuonekana kutoridhishwa na maendeleo ya miradi hiyo, ikiwemo uongozi wa Halmashauri kutokuwa na utaratibu mzuri (Modality) katika kusimamia miradi ya maendeleo hasa ile ya afya ambayo serikali imepeleka fedha.
Akiwa kwenye ukaguzi katika Zahanati ya kijiji cha Mtima ambapo utekelezaji wa mradi ulisimama kwa zaidi ya mwaka mmoja licha ya serikali kupeleka kiasi cha shilingi milioni 50 huku wanannchi wakichangia nguvu kazi ya Milioni 20 kwa ajili ya kumalizia boma na matundu mapya ya vyoo.
Seneda alibaini kutokuwepo kwa utaratibu mzuri (Modality) ya usimamizi wa mradi pamoja na upotevu wa vifaa mbalimbali vilivyonunuliwa lakini vikapotelea eneo la mradi, ikiwemo boksi 41 za malumalu.
‘’ Mkurugenzi hapa ulizembea haiwezekani jengo linajengwa bila ramani wala mkataba kati ya Halmashauri na fundi, lakini kuna upotevu wa boksi 41 za malumalu,”amesema.
Aidha, Katibu Tawala Seneda awali akiwa katika Zahanati ya kijiji cha Shinji baada ya kukagua maendeleo ya mradi baada ya serikali kupeleka shilingi milioni 32.5 alibaini kutokuwepo kwa mpangilio mzuri wa taarifa za matumizi ya fedha za miradi .
Fedha hizo zilitolewa na serikali tangu mwaka 2021 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo, Mnara wa Tanki la maji, pamoja na upanuzi wa chumba cha mama na mtoto.
Kutokana na hali hiyo alitoa siku 21 kwa Mkurugenzi Mtendaji na timu yake kutoa taarifa ya kina juu ya upungufu katika miradi hiyo, ikiwemo kurejeshwa kwa vifaa vilivyopotea katika maeneo ya miradi.
Katika hatua nyingine, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi katika miradi hiyo.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu