Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Zoezi la utoaji chanjo ya uviko-19 lilianza Agousti,3,2021 ambapo hadi kufikia Juni 11,2022 watu takribani 470,000 mkoani Mwanza walikuwa wamepata chanjo hiyo angalau kwa dozi ya kwanza.
Wakizungumza na timesmajira kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi jijini hapa waliopata chanjo ya uviko-19,wamewahimiza wananchi wengine kuendelea kujitokeza kuchanja chanjo hiyo kwa ajili ya kupambana na corona kwani chanjo hiyo inatolewa bure.
Ahmed Juma, ameeleza kuwa yeye alichanja chanjo mara mbili awamu ya kwanza na awamu ya pili na yupo vizuri kiafya hajapata madhara yoyote kutokana na chanjo hizo.
“Mimi nimechanja chanjo ya uviko-19 awamu mbili na tangu ni chanje sijaona madhara yoyote mpaka sasa hivi na chanjo hizo nimepata bure wala sijalipia na sijawai kuombwa fedha kwa ajili ya kupata huduma hiyo,”ameeleza Juma.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Pamba Edwin Ngonyani, ameeleza kuwa serikali kupitia vyombo vyake walifika shuleni na kutoa elimu kisha kuweka programu ya walimu kuchanja ambao waliitikia muitikio na kuchanja.
Mwalimu Edwin, ameeleza kuwa bila chanjo baadhi ya huduma mtu anaweza asizipate mfano akitaka kusafiri kwenda nje ya nchi hatoweza kupita kwenye mipaka bila kuwa amepata chanjo hiyo.
“Mimi nimechanja chanjo aina ya Johnson Johnson kwani inasaidia mtu akipata kirusi cha corona chanjo inapambana nacho pia kwa sasa watu wanasafiri kimataifa hivyo ukichanjwa kupita katika mipaka itakuwa ni rahisi na ukiumwa unakosa kipato lakini ukichanjwa unakuwa na afya unaendelea na shughuli za kutafuta kipato,”ameeleza Mwalimu Ngonyani.
Kwa upande wake mmoja wa wavuvi wa mwalo wa Butuja, Emmanuel Nyagwesi,ameeleza kuwa awali wakati zoezi la utoaji chanjo ya uviko-19 limeanza nchini hakuwa tayari kuchanjwa kwa sababu alikuwa hajapata elimu wala uelewa wa chanjo hiyo.
Ila baada ya kuelimishwa juu ya chanjo hiyo na kutambua kuwa ni muhimu katika kujikinga na kupambana na uviko-19 aliamua kuchanja na tangu apate chanjo hiyo hakuna mabadiliko yoyote yenye athari katika mwili wake kama ambavyo watu walivyokuwa wanazungumza.
Akizungumza na timesmajira Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza Amos Kiteleja, ameeleza kuwa katika zoezi la utoaji chanjo ya uviko-19 lilianza Agousti 3,2021,ambapo tangu kuanza kwa zoezi hilo mpaka Juni 11,2022 wameweza kuwachanja takribani watu 479,094 angalau kwa dozi ya kwanza huku malengo hadi kufikia Desemba ni kuchanja watu zaidi ya milioni 1.2 sawa na asilimia 70.
More Stories
Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba
Ng’ombe 10 wamekufa kwa kupigwa na radi