November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

13 wanashikiliwa tuhuma za mauaji

Na George Mwigulu,TimesMajiraOnline, Katavi.

JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi linawashikiria watu 13 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya mauaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo wakiwa na silaha wanazotumia kutekeleza uhalifu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi wa mkoa huo,ACP Kaster Ngonyani akizungumza na waandishi wa habari amesema kwenye msako uliofanyika kwa kipindi cha Mwenzi Oktoba,2023 wamefanikiwa kukamata watuhumiwa 196 wa makosa mbalimbali kati yao 13 kwa matukio ya mauaji.

Kaster ameeleza kuwa watuhumiwa hao walikutwa na vielelezo ambavyo ni nondo vipande viwili, panga, marungu pamoja na bajaji moja aina ya TVS yenye namba ya usajili MC 643 DCE wanayotumia kwa ajili ya usafiri kutoka eneo la tukio mara baada ya kumaliza kutenda uhalifu.

“Watuhumiwa hawa bado wanaendelea kuhojiwa na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamaji kujibu tuhuma hizo,”amesema.

Wakati huo huo,Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 11 wakiwa na madawa ya kulevya yanayodhaniwa kuwa ni bangi kiasi cha kete 43 sawa na gramu 22, Watuhumiwa 9 wakiwa na nyara za serikali jino moja na vipande vinne vya mnyama pori aina ya tembo pamoja na watu 12 wamekamatwa wakiwa na lita 420 za pombe haramu ya moshi.

Kamanda huyo amesema watu 158 wamekamatwa kwa kujihusisha na matukio ya wizi, unyang’anyi, uporaji, uvunjaji, uzembe na uzururaji ambapo wamekutwa wakiwa na mali za wizi baadhi yake ni pikipiki moja aina ya Sang Lg namba MC 695 BPU,Laptop mbili,Radio sabufa sita na shata za alminiam bando tatu.

“Baada ya zoezi la usalimishaji silaha haramu kwa hiari kumalizika tumeanza kufanya misako kwa wale waliokaidi kuzisalimisha kwa hiari na tumefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja na silaha aina ya gobore,”amesema.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 148 ambapo watuhimiwa 74 wamehukumiwa vifungo gerezani,watuhumiwa 22 wamehukumiwa kulipa faini,Watuhumiwa 6 wameachiwa huru na 46 bado kesi zinaendelea mahakamani.

Aidha Kaster amewashukuru wananchi kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika nyanja mbalimbali katika kukabiliana na uhalifu kwani uhalifu hauvumiliki kwa sababu unarudisha nyuma maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla.