December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto zaidi ya milioni 3 kupata chanjo ya polio kwenye mikoa 6 nchini

Na Joyce Kasiki,Timesmajira Dodoma.

WIZARA ya Afya kwa kushirikiana Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau wa Sekta ya Afya inatarajia kuendesha Kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto zaidi ya Milioni 3.2 walio na umri chini ya miaka nane ili kuwakinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo ambao tayari mtoto mmoja amethibika kuwa na maambukizi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni hiyo inayotarajiwa kuanza kutolewa kwenye Mikoa sita ya Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema,kampeni hiyo ni kufuatia kuwepo kwa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja Sumbawanga katika mkoa wa Rukwa ambaye alipooza ghafla na tayari amethibitika kimaabara kwamba ana virus vya polio.

“Kampeni hii tunaanza na mikoa hiyo sita kwanza kwa sababu imezungukwa na nchi za Burundi ,Zambia na Demokrasia ya Congo,na kufuatia hali hii Tanzania inakuwa katika hatari ya kupata maambukizi  ya polio hasa katika mikoa iliyozungukwa na nchi hizo.”amesema Ummy na

Kwa mujibu wa Ummy taarifa za kitakwimu zinaonyesha kuwa akiwepo mtoto mmoja mwenye ugonjwa wa polio ,nyuma yake kunakuwa na watoto 200 wenye polio ambapo mmoja anaweza kupata ulemavu wa kudumu na kwamba katika kila watoto kumi mtoto mmoja ataonyesha dalili za ugonjwa huo.

 “Kwa hiyo napenda nichukue fursa hii kuwataarifu kuwa tutakuwa na Kampeni maalum ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya Polio (nOPV2) kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka minane ambayo itafanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 21 – 24 Septemba, 2023 katika mikoa hiyo sita kampeni ambayo itafanyika nyumba kwa nyuma,katika mikusanyiko na nyumba za Ibadan a shuleni,

 “Lengo la kampeni hii ni kuwafikia watoto 3,250,598 waliozaliwa baada ya mwaka 2016 ili kuwakinga dhidi ya Kirusi cha Polio aina ya pili  kinachoweza kusababisha ulemavu wa kudumu ambapo kwa mkoa Rukwa tunatarajia kuwafikia watoto 391,883 Kagera 729,387 Kigoma 884,477 Mbeya 614,346 Katavi 227,862 na Songwe 402,643”.  amefafanua Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema Ili kufanikisha Kampeni hii, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI pamoja na Wadau wa chanjo imeshafanya maandalizi kwa ajili ya kuwezesha zoezi bila kuathiri shughuli zingine za wananchi.

“Wakati wa Kampeni kutakuwa na jumla ya timu yenye jumla ya watoa huduma za afya 5,291 kwa Mikoa yote sita itakayofikiwa na zoezi hili ambapo kila timu itakuwa na watoa huduma watatu. Timu hizi zitakuwa zinatoa huduma ya chanjo kwa walengwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya, nyumba kwa nyumba, shuleni na maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ikiwemo Nyumba za Ibada”. 

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za afya ili kuwezesha watoto wao kuchanjwa kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba huku akiuhakikishia umma kuwa chanjo hiyo ni salama.

Vile vile amewataka waganga wakuu wa Mikoa kuhakikisha chanjo zipo za kutosha ili watoto wote waliolengwa waweze kufikiwa lakini pia amewataka waimarishe maelekezo ya utoaji elimu kwa umma ili jamii ielewe kuhusu kampeni ya chanjo hiyo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema katika kuendeleza mikakati ya kutoa chanjo dhidi ya Polio, imeundwa timu ya watu waliopata mafunzo ya kutoa chanjo hiyo katika Mikoa hiyo sita.

“Tumeunda timu nzuri ambayo imepata mafunzo ya kutoa chanjo ambayo ina  watoa huduma Elfu Tano Mia Mbili Tisini na Moja  katika Mikoa hiyo Sita ili kuhakikisha watoto wote wanafikiwa katika kupatiwa Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio” amesema Prof. Nagu amesema na kuongeza kuwa

“Tunawapa hamasa wazazi wahakikishe kwamba, wanawatoa watoto wao kupata chanjo hii ili kuwaepusha watoto wetu kupata ulemavu ambao kwakweli unakingika kwa kutumia chanjo”. Ameongezea Prof. Nagu.

Tanzania inaendesha Kampeni hiyo ya chanjo kutokana na Wizara kupokea taarifa mnamo Mei 26, 2023 za uwepo wa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja ambaye alionyesha dalili za kupooza kwa ghafla. 

Mtoto huyo ambaye alitolewa taarifa kutoka Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa. Uchunguzi wa Maabara umethibitisha kuwa mtoto huyo ana maambukizi ya virusi cha Polio.