November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto wa kiume 11 wafanyiwa ukatili wa kingono

Na Patrick Mabula,TimesMajira Online,Kahama

WATOTO wa kiume 11, wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono katika matukio 132 yaliyoripotiwa Halmashauri ya Mji Kahama mkoani Shinyanga kwa kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Halmashauri ya Mji Kahama kwenye kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zilizofanyika kimkoa wilayani hapa, kipindi cha Januari hadi Septemba mashauri 1,627 ya ukatili yaliripotiwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji Kahama, Abrahamani Nuru alisema kati ya matukio hayo 69 yalikuwa ya watoto kati ya hayo 58 ni watoto wa kike na 63 ni ya wanawake watu wazima.

Amesema kwa kipindi hicho, waliweza kupokea mashauri ya ndoa za utotoni nane kwa mujibu wa taratibu waliyafikisha kwenye vyombo vya dola kwa hatua na kuyapeleka mahakamani manne na tayari matatu yalishatolewa hukumu.

Nuru amesema kwa upende wa mimba za utotoni, kulikuwa na matukio 35 na kati yake 18 yalifikishwa mahakamani na 11 tayari yalishatolewa hukumu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisolikuwa la kiserikali la Huheso Foundation, Juma Mwesigwa linalojishughilisha ukatili katika mradi wake wa mwanamke amka kupitia ufadhili wa The Foundation for Civil Society alisema, mfumo dume katika jamii mkoani Shinyanga bado ni tatizo na ndiyo chanzo cha vitendo vya ukatili wa jinsia.

Amesema kupitia mradi huo wa Mwanamke Amka, wanafanya kazi ya kutoa elimu kupitia kituo cha redio ya shirika hilo pamoja na watumishi wa umma, kupitia Kamati za Mtakuwwa katika maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini ili kutokomeza vitendo hivyo.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Tellack, alisema ukatili wa kijinsia umekuwa ukifanywa kwa wanaume baada ya kuwawezesha kiuchumi, wanawake wanapofanikiwa huwafanyia vitendo hivyo.

Alisema kutokana na elimu ya ukatili wa kijinsia inayotolewa na serikali na mashirika binafsi, ameanza kupokea malalamiko kutoka kwa wanaume ya kufanyiwa vitendo hivyo na wanawake na kuwataka kuacha tabia hiyo ya kuwa wanalipiza kisasi, wanapopata mafanikio kiuchumi bali iwe chachu ya kuzidisha upendo na amani na kutunza familia zao.