December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto 22,000 waondolewa katika mashamba ya tumbaku

Na Allan Vicent,Timesmajira Online. Tabora

JUHUDI za kupambana na vitendo vya utumikishwaji watoto katika mashamba ya tumbaku zilizofanywa na miradi ya Prosper, zimefanikiwa kuokoa watoto 22,000 waliokuwa wakitumikishwa katika kazi hatarishi kwenye mikoa mitatu nchini.

Hayo yamesemwa jana na Meneja wa Mradi wa Proser Reset, Fredrick Malaso katika Maadhimisho ya Siku ya Kutokomeza Utumikishwaji Watoto Duniani, yaliyofanyika kimkoa katika Kijiji cha Mtakuja/Igagala namba 5 Kata ya Igagala wilayani Kaliua Mkoa wa Tabora.

Amesema mafanikio hayo, yamepatikana kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na miradi ya Prosper kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali katika kutokomeza vitendo hivyo kwa vipindi tofauti kati ya mwaka 2011 na 2020.

Ameongeza kuwa wazazi na walezi 400, walipata elimu ya kusoma na kuandika, vijana 1,600 walipewa elimu ya ufundi stadi na kaya 1,500 ziliwezeshwa mikopo na kuanzisha biashara ndogo ndogo ili kuinua uchumi wao.

Amefafanua miradi hiyo kuwa ni Prosper, Prosper Plus na Prosper Umoja ambayo ilitekelezwa katika Mikoa ya Tabora, Mbeya na Songwe ambapo jumla ya wilaya tano kwenye mikoa hiyo ilinufaika na sasa wameanza mradi wa Prosper Reset.

“Tathmini inaonesha kupitia miradi hiyo, hali ya utumikishwaji watoto katika mashamba ya tumbaku imepungua kwa zaidi ya asilimia 84.3 katika mikoa hiyo, tunapongeza kazi nzuri iliyofanyika na sasa tunahitaji ushirikiano zaidi,” amesema.

Amepongeza kuwa Serikali ya Wilaya na Mkoa wa Tabora kwa kutambua mchango na juhudi kubwa zinazofanywa na asasi za kiraia na kuziunga mkono katika kutoa elimu na misaada kwa wazazi na walezi wa watoto ili kupunguza umaskini.

Amesema utafiti uliofanyika mwaka 2014 nchini (Tanzania Integrated Labor Force Survey (TILFS), ulionesha vitendo vya utumikishwaji kuathiri watoto milioni 4.2 wenye umri wa miaka 5-17 kati ya watoto milioni 15, sawa na asilimia 29.3 na asilimia 94 ya matukio mengi ya utumikishwaji yanafanyika katika sekta ya kilimo.

Malaso amesema\ mradi mpya wa Prosper Reset, utatekelezwa kwa miaka mitatu katika wilaya tano za mikoa hiyo ambazo ni Kaliua, Sikonge na Urambo (Tabora), Wilaya ya Chunya (Mbeya) na Wilaya ya Songwe mkoani Songwe.

Ametaja malengo ya mradi huo kuwa ni kuwezesha vikundi vya kuweka na kukopa (VSLA), vikundi vya vijana vya mashamba darasa (MFS) na vile vya ufundi stadi kwa kuvipa elimu ya usimamizi wa biashara na kuweka akiba.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Abel Busalama amepongeza asasi za TDFT na TAWLAE zinazofadhiliwa na Mfuko wa Eliminating Child Labour in Tobacco Growing Areas (ECLT) na washirika wao kwa juhudi kubwa za kupinga utumikishwaji watoto katika kilimo cha tumbaku.