December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto 194 wapewa mimba ndani ya mwezi mmoja

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Momba.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amesema kuwa ndani ya mwezi mmoja jumla ya watoto 194, wakiwemo wanafunzi katika Wilaya ya Momba wamepewa mimba.

Kufuatia hali hiyo ametoa siku 21 kwa Mkuu wa Wilaya ya Momba, Kenani Kihongosi  kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha watu wote waliohusika na vitendo hivyo wanasakwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Kapele kwenye  mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo mei 15, 2024, Mkuu huyo wa Mkoa alisema hali hiyo haikubaliki na ni aibu kubwa kwa viongozi wa Wilaya hiyo.

“Kwenye hili hatuna masihara hata kidogo na Mkuu wa Wilaya nataka hawa waliongiza mimba kwa hawa watoto 194 tuone nao wanaingizwa kwenye vyombo vya sheria na baada ya  siku 21 nataka nipate majibu mmefika wapa, hatuwezi kuleana na mambo ya namna hii”.

“Mikoa mingine wenzenu wanapeleka watoto shule nyie mnaacha watoto wenu wa kike wanapewa mimba na kuolewa mapema na mnafurahia hivyo vitendo… hili halikubaliki na sisi viongozi hatujaletwa hapa kuja kusindikiza watoto wadogo kwenda kuolewa”aling’aka Mkuu wa Mkoa Chongolo.

Aidha, Chongolo alitumia jukwa hilo kuwataka watendaji wa Vijiji na Kata kuhakikisha  watu wanaoshiriki vitendo vya kuwapa mimba na vitendo vya ukatili kwa watoto wadogo.

“Nyie mnajua kila mtoto kwenye maeneo yenu mtoto akipata mimba halafu hakuna aliyechukuliwa hatua na nyie mtawajibika kwa kuwa mtakuwa hamjatusaidia”. Aligiza Chongolo.