January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoa huduma sekta ya utalii Watakiwa kualika wawekezaji kukuza sekta ya utalii

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa Mkoa wa Mwanza una vivutio vingi ikiwemo wanyama pori, fukwe za ziwa Victoria, maeneo mbalimbali ya kihistoria, uchimbaji wa madini, utamaduni na vivutio vingi kadha wa kadha, ambavyo kwa pamoja vinachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Mkoa huo.

Hivyo wataalamu katika sekta ya utalii mkoani Mwanza wametakiwa kualika wawekezaji ili waweze kuwekeza katika sekta ya utalii mkoani humo ikiwemo kutengeneza fukwe ndani ya ziwa Victoria.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa watoa huduma katika sekta ya utalii yanayohusu mwongozo wa kukabiliana na Uviko-19 katika sekta ya utalii nchini ambayo yameanza Machi 7 hadi 11 mwaka huu, yanayofanyika mkoani hapa ambayo washiriki 150 wanatarajia kunufaika na mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli amesema,sekta ya utalii ni muhimu katika kukuza pato la taifa.

Hivyo ni fursa ambayo wawekezaji wanaoaswa kualikwa ili waweze kuwekeza mkoani Mwanza katika sekta ya utalii

Ambapo wataalamu hao wanajukumu la kukuza mji wa Mwanza hususani katika kukuza sekta ya utalii.

Kalli amesema,sekta ya Maliasili na Utalii imeendelea kuchangia katika kuingiza fedha za kigeni na pato la taifa (GDP) kupitia utalii, ajira, nishati, elimu, utafiti, utamaduni, burudani na tiba.

Ambapo pia sekta hiyo huchangia takribani asilimia 25 ya fedha za kigeni na zaidi ya asilimia 17 katika pato la taifa.

Amesema,wananchi wengi wameendelea kushiriki kwenye shughuli za utalii ambapo sekta ya utalii imeweza kuchangia ajira takribani milioni 1.6 za moja kwa moja na zile ambazo sio za moja kwa moja.

“Takwimu hizi ni chachu kwetu wanaMwanza kuendelea kuongeza na kuimarisha shughuli za utalii katika Mkoa wetu kwa kuboresha utoaji wa huduma katika biashara zetu za utalii,” amesema Kalli.

Mbali na hayo Kalli amesema,janga la UVIKO-19 limeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii duniani zikiwemo nchi ambazo ni masoko makuu ya utalii, kwa upande wa Tanzania idadi ya watalii waliotembelea nchini ilipungua kutoka 1,527,230 mwaka 2019 hadi 620,867 mwaka 2020 sawa na upungufu wa asilimia 59.3.

Mapato yatokanayo na Utalii yalipungua kutoka Dola za Marekani Billioni 2.6 mwaka 2019 hadi Dola za Marekani Billioni 0.715 mwaka 2020 sawa na upungufu wa asilimia 72.5.

“Tumeshuhudia kuyumba kwa biashara za utalii na hata kufungwa kwa baadhi ya makampuni ya utalii na mahoteli, kwa sasa sekta ya utalii nchini imeanza kuimarika kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia,”amesema Kalli.

Akizungumzia mafunzo hayo Kalli amesema, matarajio ya Serikali ni kuwa mafunzo hayo yatakapokamilika yatachangia kuboresha utoaji huduma katika mnyororo wa utalii na kupelekea nchi kuongeza idadi ya watalii na kufikia malengo ya kupata watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025.

“Ninapenda kuwasisitiza washiriki kuhakikisha mnafaidika kikamilifu na mafunzo haya ili kuleta tija katika sekta yetu ya utalii,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt.Shogo Mlozi,amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta ya Utalii na katika juhudi za kuleta suluhu ya changamoto zilizoikumba sekta hii, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, chini ya Chuo cha Taifa cha Utalii, imeandaa mafunzo kwa wadau wakuu wa sekta ya Utalii na Ukarimu na watoa huduma katika mnyororo mzima wa utalii.

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa UVIKO-19 awamu ya kwanza kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19.

“Mafunzo kwa waendesha biashara za Utalii na Ukarimu yameshafanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Njombe, Ruvuma, Iringa, Mbeya na kwa sasa yanaendelea hapa mkoani kwetu Mwanza na mkoa jirani wa Mara ambayo yatawajengea uwezo watoa huduma za utalii nchini juu ya namna bora ya kukabiliana na janga la UVIKO-19 kwa kuzingatia matakwa ya kiafya na usalama,”amesema na kuongeza kuwa

“Pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa na hatimaye kuimarisha ushindani wa nchi katika masoko mbalimbali, ikiwemo kuvutia watalii wa kimataifa kuja nchini hasa katika kipindi hiki cha mtazamo mpya wa utoaji huduma za utalii na usafiri kukabiliana na UVIKO-19,pia yanalenga kuhakikisha kuwa watanzania wanaofanya kazi katika Sekta ya Utalii wanakuwa salama,”.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Ofisa Uhifadhi Daraja la pili,Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane Hilda Mikongoti amesema, mafunzo hayo ni fursa nzuri ambayo wameipata kwani wamejifunza jinsi gani ya kujikinga wao wanaotoa huduma kwa watalii wanao watembelea na wanawakingaje na janga hilo la UVIKO-19.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Shogo Mlozi, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa watoa huduma katika sekta ya utalii yanayohusu mwongozo wa kukabiliana na UVIKO-19 nchini kwa Mkoa wa Mwanza ambayo yanafanyika mkoani hapa.picha na Judith Ferdinand
Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa watoa huduma katika sekta ya utalii yanayohusu mwongozo wa kukabiliana na UVIKO-19 nchini kwa Mkoa wa Mwanza ambayo yanafanyika mkoani hapa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.picha na Judith Ferdinand
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku tano kwa watoa huduma katika sekta ya utalii yanayohusu mwongozo wa kukabiliana na UVIKO-19 nchini kwa Mkoa wa Mwanza ambayo yanafanyika mkoani hapa.picha na Judith Ferdinand