Ni kupitia Mgodi wa GGML, waipongeza Serikali
Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Watoa huduma kwenye migodi ya madini katika mkoa wa Geita wameendelea kunufaika kupitia Sekta ya madini kupitia utoaji wa huduma kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) uliopo mkoani Geita na kuwataka watoa huduma wengine wenye vigezo kuendelea kujitokeza na kuchangamkia fursa zilizopo katika migodi ya madini.
Watoa huduma hao waliyazungumza hayo kwa nyakati tofauti Novemba 30, 2022 kwenye mahojiano ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia mchango wa Sekta ya Madini katika kuwawezesha watanzania kiuchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii.
Jeremiah Musa ambaye ni meneja wa kampuni ya Bluecoast-Geita inayojihusisha na utoaji wa huduma ya usambazaji wa mafuta pamoja na usafirishaji katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita alisema kuwa, mara baada ya Serikali kuboresha kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, walipata mafunzo kupitia Baraza la Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi (NEEC) na kubaini fursa za utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini na vigezo na kupata zabuni katika mgodi wa GGML ya usambazaji wa mafuta na usafirishaji.
Alisema kuwa, kupitia zabuni hiyo katika mgodi wa GGML kampuni yake imeweza kutoa ajira zaidi ya 500 na kuiomba Serikali kuendelea kuwajengea uwezo watanzania ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye Sekta ya Madini.
Katika hatua nyingine, aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa kuendelea kuboresha kanuni za madini na kutoa elimu kwa wadau wa madini kupitia makongamano, maonesho na mikutano mbalimbali na kusisitiza kuwa kampuni yake imejipanga zaidi ili kuweza kutoa huduma zaidi kwa migodi mingine ya madini nchini.
Naye Adam Rajab ambaye ni msimamizi wa kampuni inayotoa huduma za chakula na malazi katika mgodi wa GGML aliongeza kuwa sambamba na kampuni yake kutoa ajira zaidi ya 300 kwa wakazi wanaozunguka mgodi huo, wametoa elimu ya namna ya kuzalisha bidhaa bora za vyakula kwa wananchi wanaoishi jirani na mgodi hali iliyofungua fursa zaidi kwa wananchi hao huku Serikali ikiendelea kupata kodi mbalimbali.
Wakati huohuo Mwenyekiti wa Soko la Dhahabu la Geita, Dotto Zanzui sambamba na kuishukuru Serikali na Mgodi wa GGML kwa uanzishwaji wa soko hilo alifafanua kuwa soko limekuwa mkombozi kwa kuwa wameweza kuuza madini yao kulingana na bei elekezi inayotolewa na Tume ya Madini yenye kuendana na soko la dunia.
“Kabla ya uanzishwaji wa soko hili la madini, tulikuwa hatuna bei rasmi ya madini, usalama ulikuwa ni mdogo sana lakini kwa sasa tunaweza kuuza madini yetu na kupata faida kubwa huku Serikali ikipata kodi mbalimbali,” alisisitiza Zanzui
More Stories
Waziri Lukuvi aeleza maono ya Isimani ijayo
Madiwani Korogwe TC wahakikishiwa maji ya uhakika
CHADEMA wampongeza Mkurugenzi Mpanda