Na Patrick Mabula,Timesmajira. Online, Ushetu
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama, Gagi Lala amewataka watendaji kuzingatia ushauri unaotolewa na Baraza la Madiwani katika kuisimamia halmashauri, wanapotimiza wajibu wao wa kazi kwenye kuwatumikia wananchi.
Lala ametoa agizo hilo hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Maalumu cha Madiwani cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu ya Serikali (CAG ) na kuwataka watendaji, kufanya kazi kwa kuzingatia maelekezo ya baraza ili kupunguza hoja za CAG zilizofanya kupata hati yenye mashaka.
“Baraza la Madiwani katika vikao vyake, limekuwa likitoa maelekezo na ushauri mbalimbali kwa watendaji, tunawaomba mnapotimiza wajibu wenu wa kazi kuzingatia ushauri wetu tuweze kumaliza hoja za CAG, ambazo zimekuwa zikiongezeka kila mwaka,” amesema Diwani wa Viti Maalumu, Esther Matone.
Diwani huyo amesema, kutokuzingatiwa ushauri wao wanaotoa katika vikao kumesababisha kuendelea kuongezeka kwa hoja za CAG toka hoja nane za mwaka 2016/17 na kuwa hoja 53 kwa mwaka 2019/20 na kusababisha Halmashauri ya Ushetu kupata hati yenye mashaka.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyakende, Doa Magingi amesema hati yenye mashaka waliyoipata inawaweka katika mazingira mabaya ya uwakilishi wao kwa wananchi na kuwataka watendaji waliosababisha hali hiyo, kujirekebisha kabla hawajaamua kuwachukulia hatua.
“Haipendezi hata kidogo kuona uzembe unafanywa na watendaji, wakati wanajua wajibu wao wa kazi na kusababisha kuendelea kuongezeka kwa hoja za CAG na kuwataka wanaohusika, kuacha mara moja kufanyakazi kwa mazoea,” amesema Robart Mihayo ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyamilangano.
Diwani wa Kata ya Iguda, Tabu Katoto amehoji kipengele cha moja ya hoja za CAG kuhusu gharama ya kutengeneza milango ya Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu, ambayo pia Madiwani walishatilia shaka juu ya gharama halisi katika utengenezaji wa milango kwa sh. 700,000 kila mmoja na kuomba wapewe majibu.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Serikali za Mitaa wa Mkoa wa Shinyanga, Alphonce Kasanyi amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kubadilika na kuacha kufanyakazi kwa mazoea na wafanyekazi kwa mshikamano, kama timu mmoja katika utendaji wao na kuwaagiza kuhakikisha wanajibu mapema hoja za CAG zilizosababisha kupata hati yenye mashaka.
Akizungumzia kuhusu changamoto hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Wandele Lwakatare amekiri kuwepo kwa upungufu katika utendaji kwa baadhi ya watumishi na kuahidi kuyafanyia kazi yale yote yaliyosababisha, kuongezeka kwa hoja za CAG kwa kuzingatia ushauri wa Barza la Madiwani.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi