January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watendaji SMZ watakiwa kuacha ubinafsi katika utendaji kazi

Na Haji Mtumwa, TimesMajira Online

Zanzibar. Watendaji wa wizara ya Ardhi,Maendeleo ya Makaazi na Wizara ya Maji,Nishati na Madini wametakiwa kuacha ubinasi katika utendaji wa kazi zao ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya serikali ambayo ni chachu ya maendeleo.

Ameyasema hayo waziri wa Nishati,Maji na Madini, Shahibu Hassan Kaduara wakati wa makabidhiano ya Wizara hiyo na Waziri wa Ardhi,Maendeleo ya Makaazi Rahma Kassim Ali huko Maisara Mjini Unguja.

Amesema ukusanyaji mzuri wa mapato ya serikali yanayotokana na rasilimali zilizopo unatokana na utendaji mzuri wa wafanyakazi hivyo wafanyebidiii ili serikali iweze kupiga hatua.

Alisema si jambo zuri hata kidogo kuona baadhi ya watendaji kujiona wao ni Bora kuliko wengine ama kwa vyema au nafasi walizonazo,kitendo ambacho hakikubaliki hata kidogo.

“Niwaombe sana watendaji wenzangu tuwe ni wenye mashirikiano na kuachana na tabia za kujiona wewe Bora kuliko wenzako, kitendo ambacho hata RAIS wetu anakikemea sana”alisema

Amesema mashirikiano ya pamoja ni nguzo imara ya kukuza maendeleo katika taasisi hivyo kila moja atambue wajibu wake katika kazi ili kukuza utawala bora.

Aidha amesema wakati umefika sasa kwa zanzibar kubadilika kimaendeleo na yale malengo ya rais yaweze kufikiwa katika kutimiza ahadi za wananchi za kujenga nchi katika kiwango kilichobora hasa kwenye sekta ya miundombinu ya maendeleo na makaazi.

Nae Waziri wa Ardhi,Maendeleo na Makaazi Rahma Kassim Ali amewataka watendaji hao kutoa mashirikiao ya dhati kwa viongozi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika serikali ili jamii iweze kuneemeka na maendeleo ya nchi yao.

Amesema watendaji waache tabia ya kila mmoja kujiona bora kuliko mwengine kwani maendeleo hayawezi kuletwa na mtu mmoja mmoja badala yake kwa mashirikiano.

Kwaupande wao Makatibu wakuu wa wizara hizo mbili Joseph Kilangi na Dr Miraji Ngereza wameahidi kufanyakazi kwa bidii na mashirikiano kwalengo la kusaidia wananchi kupata maendeleo bora ambayo ni haki yao ya msingi.

Wamesema nguvu zaidi zinahitajika katika kutimiza malengo ya serikali hivyo nivyema watendaji kwa kushirikiana na viongozi wakawajinika kwa bidiii.