December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watendaji watakiwa kukomesha kabisa mimba za utotoni

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

WATENDAJI wa Vijiji na Kata,Halmashauri ya Wilaya ya Songwe wametakiwa kufanya mikutano katika maeneo yao ili kuelezea shughuli mbalimbali za maendeleo zilizotekelezwa na ambazo zinaendelea kutekelezwa na serikali, ikiwemo kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto wao shule na kusimamia maendeleo yao .

Maelekezo hayo yametolewa ikiwa ni mikakati mahususi itakayosaidia kuwaepusha watoto hao na mimba za utotoni,ambapo Mkoa wa Songwe unatajwa kuongoza nchini kwa mimba za utotoni.

Maelekezo hayo yametolewa Disemba 11, 2023 na Katibu Tawala (RAS)wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda, wakati akizungumza na watumishi wa Tarafa ya Kwimba, Wilayani humo, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kupitia na kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa huo.

Baada ya kusikiliza changamoto mbalimbali zilizoibuliwa na watumishi katika kikao hicho, ndipo Katibu Tawala  akatumia fursa hiyo kuwataka wenyeviti wa hao vijiji na kata kuitisha na kufanya mikutano katika maeneo yao kwa lengo la  kueleza mambo mbalimbali ya maendeleo  yanayofanywa na serikali.

“Fanyeni mikutano ya kijiji Kwani mikutano hiyo ni muhimu sana kwa ajili ya kuwaambia wananchi ni kitu gani serikali imefanya katika maeneo yao Kwani siku hizi kuna mambo mengi serikali inafanya” ameeleza Seneda.

Aidha, Katibu  Tawala huyo amewataka watendaji hao kutumia mikutano hiyo kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa elimu ambapo itasaidia  wazazi kuona umuhimu wa kupeleka watoto shule.

“Kupitia mikutano hiyo ya vijiji mtaweza kuhamasisha wazazi kuhakikisha kwamba wanawapeleka watoto wao shuleni na kuwasimamia ili waweze kufanya vizuri badala ya kuwacha bila usimamizi na matokeo yake kuchoropoka na kwenda kufanya shughuli mtaani na matokeo yake kuishia kupata mimba za utotoni” amesisitiza Seneda.

Seneda amesema hali ya mdondoko kwa wanafunzi katika Mkoa wa Songwe ni mkubwa ambapo wanafunzi 10,000 hawakuweza kufanya mitihani ya kumaliza darasa la saba kwa mwaka huu wa 2023 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni.

Kiwango kikubwa cha mdondoko katika Mkoa huo wa Songwe kwa sehemu kumechanguwa na Wilaya ya Songwe ambapo wanafunzi wengi hukatiza masomo na kwenda kufanya kazi kwenye maeneo ya uchimbaji wa dhahabu, kilimo na shughuli za uvuvi.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan akizindua ripoti ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto pamoja na viashiria vya malaria Tanzania ya mwaka 2022, alisema pamoja na Tanzania kuendelea kupunguza viwango vya mimba za utotoni kutoka asilimia 27 mwaka 2015/2016, aliitaja mikoa mitano vinara wa mimba za utotoni.

Alitaja Mikoa hiyo na asilimia zake kwenye mabano kuwa ni  Mkoa wa Songwe (45),  Ruvuma (37), Katavi (34),  Mara (31), pamoja na Rukwa (30).