November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wateja TANESCO watakiwa kuendelea na maboresho

Na Cresensia Kapinga, TimesMajira Online, Songea 

WATEJA wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Kanda ya Kusini na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi wametakiwa kuendelea na na maboresho ya mfumo wa LUKU hadi Novemba 24 Mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano wa shirika hilo Mjini Songea Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa uma wa TANESCO, Iren Gowele alisema kuwa maboresho hayo yanalenga kuendana na viwango vya mifumo ya LUKU ya Kimataifa na kuongeza ufanisi zaidi pamoja na usalama wa mita za LUKU nchini.

Gowele alisema zoezi hilo la mfumo wa LUKU linaanza rasmi Juni 24, mwaka huu katika mikoa ya Mtwara Lindi, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Rukwa, Njombe na Songwe hivyo  amewashauri wateja wa shirika hilo kujitokeza ili kufanikisha zoezi hilo.

Gowele alifafanua kuwa mteja atakapo nunua umeme kwa mara ya kwanza kuanzia tarehe tajwa atapokea tarakimu kwenye makundi matatu, ambapo kila kundi likiwa na tarakimu 20 .

Alieleza zaidi kuwa kundi la 1 na la 2 la tarakimu litakuwa kwa ajili ya maboresho na kundi la 3 litakuwa la tarakimu za umeme na mteja ataingiza tarakimu la kila kundi kwa mfuatano unao someka kwenye risiti ya malipo au ujumbe mfupi wa simu.

Alisema kila atakapo ingiza kundi moja mteja atapaswa kubonyeza alama ya kukubali ya reli # au mshale wa kukubali hapo atakuwa amefanikiwa kuboresha mita yake na kupokea kiwango cha umeme alioununua.

Alisema zoezi hilo ni bure na litafanyika mara moja tu kwa mteja baada ya kufanya hivyo atakuwa amefanya maboresho.

Hata hivyo, Gowele alisema baada ya Mikoa ya Kanda ya Kusini na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi zoezi hilo litaendelea kwa mikoa mingine nchini kwa awamu kadri TANESCO itakatangaza.

Iren Gowelle akizungumza na waandishi wa habari juu ya mabadiliko ya mita za Luku kwenye ukumbi wa Tanesco Manispaa ya Songea.