December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watatu kati ya saba waliokamatwa na dawa za kulevya kilogramu 3,182 wafikishwa Mahakamani

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

WAKAZI watatu wa Kigamboni jijinii Dar es salaam, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilogramu 882.71 na Methamphetamine zenye uzito wa kilogramu 2167.29.

Washitakiwa hao ni mfanyabiashara Najim Mohamed (52), mfanyabiashara, Maryam Mohamed (50) na Juma Abbas (37) ambaye ni msaidizi wa kazi za ndani.

Akisoma Mashtaka yao leo Disemba 29,2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Aaron Lyamuya, wakili wa serikali mwandamizi Hemed Halfan, ameiambia Mahakama kuwa, katika shtaka la kwanza inadaiwa kuwa, Disemba 15, 2023 washtakiwa wote wakiwa katika eneo la Kibugumo shule walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilogramu 882.71.

Katika shtaka la pili alidai kuwa katika eneo hilo na siku hiyo washtakiwa hao walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa kilogramu 2,167. 29.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yanayowakabili, hakimu Lyamuya amesema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hivyo washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote hadi watakapoitwa Mahakama Kuu.

Hata hivyo, wakili Halfan, amesema upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili kutajwa.

Kesi hiyo imehairishwa hadi Januari 11, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote watatu wamerudishwa rumande kwani kesi inayowakabili haina dhamana.

Washtakiwa hao watatu ni kati ya watuhumiwa saba waliotangazwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika tarehe 27 Disemba 2023, kuhusika na jumla ya kilo 3,182 za dawa za heroin na methamphetamine.