December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania watakiwa kujichunguza Saratani

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka wananchi (wanawake kwa wanaume) kufanya uchunguzi wa awali wa kujipima Saratani ya Matiti na hasa kujipima wenyewe kila mwezi.

Waziri Ummy aliyasema hayo Jana Octoba Mosi, 2023 wakati akimuwakilisha Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwenye Maadhimisho ya Mwezi wa Saratani ya Matiti yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road Jijini Dar es Salaam. 

“Wataalamu wanatueleza kwamba mtu anaweza kujichunguza mwenyewe na akiona mabadiliko ya uvimbe katika titi, basi anashauriwa kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za Afya kwa uchunguzi zaidi”. Amesema Waziri Ummy 

Aidha, Waziri Ummy amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani takribani Elfu Arobaini na Mbili (42,000) kila Mwaka, wagonjwa asilimia 38 tu ndio wanafika Hospitali, maana yake katika kila wagoniwa 100 wa Saratani, wagonjwa 38 tu ndio wanafika katika vituo vya kutolea huduma za Afya. 

“Wakati Tanzania tunakadiriwa kuwa na wagoniwa wapya wa Saratani takribani Elfu Arobaini na Mbili (42,000) kila Mwaka, wagonjwa asilimia 38 tu ndio wanafika Hospitali, maana yake katika kila wagoniwa 100 wa Saratani, wagonjwa 38 tu ndio wanafika katika vituo vya kutolea huduma za Afya”. Amesema a Waziri Ummy 

Pia, Wazir Ummy alisema taarifa ya mwaka 2022/2023, inaonesha kuwa Taasisi ya Saratani Ocean Road ilihudumia wagonjwa wapya takriban 8,779 na asilimia 13 ya wagonjwa hao sawa na wagonjwa 1,141 walikuwa na Saratani ya Matiti.

“Saratani ya Matiti ni tatizo ambalo limekuwa likiongezeka kwa kasi hapa nchini, Mathalan mwaka 2000 Saratani ya Matiti ilikuwa imeshika nafasi ya nne (4) ya magonjwa yanayotatiza na katika mwaka 2022/23 imeshika nafasi ya pili (2) hivyo kuathiri wagonjwa wengi”. Amesema Waziri Ummy

Vile vile, Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Wizara ya Afya kufunga mashine za CT-Scan katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa na pia kuna mashine za Ultrasound zimefumgwa katika Hospitali zote za Halmashauri nchini. 

“Hii inamaanisha uchunguzi na ugunduzi wa Saratani ya Matiti ambapo unaweza kupima katika Hospitali ambazo zipo karibu na mahali tunapoishi ikiwemo Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Halmashauri”. Amesema Waziri Ummy 

Hivyo, Waziri Ummy ametoa Rai kwa wananchi kuhakikisha wanafanya vipimo katika Hospitali angalau mara moja kwa mwaka hususan kwa wanawake ili ikigundulika una tatizo basi matibabu yaanze mapema. 

“Lakini hata wanaume wanatakiwa kupima kwakuwa, katika kila wagonjwa wa Saratani ya Matiti 100, wagonjwa 99 ni wanawake na Mmoja ni mwanaume hivyo tunawaomba wananchi wawahi katika vituo vya kutolewa huduma za Afya ili kupima na kupata matibabu mapema kwa wenye changamoto hiyo”. Amesema Waziri Ummy

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Julius Mwaisalege amesema huduma za saratani zimeendelea kuboreshwa kwa ukanda wa Kusini mwa jangwa la Sahara kwa kuwa na tiba za kisasa za tiba mionzi na pia wanazo dawa za aina zote za Tiba kemia pamoja na mashine za infusion.

Aidha amesema Taasisi inajenga kituo Cha tiba ya Saratani katika hospitali ya rufaa ya Mbeya ambapo shilingi Bilioni 1.2 zimetengwa kutoka serikalini.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi, Dkt. Jerry Slaa amewataka wananchi kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa awali ili kuweza kugundua ugonjwa huo mapema zaidi hivyo kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa kutibiwa na kupona kabisa.

“Saratani ya matiti ni magonjwa yanayoua sana, alimia 86 ya wagonjwa wanaofika hospitali inakua tayari wanechelewa kwahiyo matibabu yao yamekua makubwa na hawaponi wanapoteza maisha”

“Ni vyema Kuhamasisha wananchi, kwani saratani ipo hivyo wananchi wafanye vipimo mara kwa mara ili kuweza kuwahi kupata matibabu mapema na kupona”