Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Watanzania na wadau wote wanaojihusisha na sekta ndogo ya asali wametakiwa kuchangamkia fursa ya kupeleka asali katika soko la china ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuendelea kuleta manufaa kwa watanzania.
Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Danstan Kitandula baada ya utiaji saini makubaliano kati ya serikali ya Jmahuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na serikali ya Jamhuri ya watu wa China lengo ikiwa ni kufanikisha usafirishaji wa asali kutoka Tanzania kwenda nchini China.
“Wenzetu wa china soko lao ni kubwa sana, kwa mwaka wanauhitaji wa tani 38,000,000 kwahiyo soko ni kubwa sana, nitoe rai kwa watanzaia wadau wote wanaojihusisha na sekta ndogo ya asali kwamba milango imefunguliwa waje wizarani tuweke mikakati yetu tuzungumze ili tuweze kulikamata soko la china ambalo furs hii imefunguka baada ya serikali yetu kufanya mazungumzo na wenzetu wa china kuona kwamba vikwazo vya biashara kati ya nchi hizi mbili vinaondoka ili tuweze kunufaika na sekta hii”
“Watanzania tuitumie na kuikumbatia fursa hii twende tukalikamate soko
La china ili tuweze kuuza zaidi, tuna uwezo mkubwa sana wa kuongeza uzalishaji kwasababu tuna mapori na hifadhi za misitu takribani hekta milioni 48 hivyo uwezekano wa kufuga asali na asali hiyo ikawa na ubora na ikatambulika duniani”
Hata hivyo, Kitandula alisema kwa sasa uzalishaji wa asali upo kwenye kiwango cha takribani tani 33,276 sawa na asilimia 24.1 ya uwezo uliopo. Kiwango hiki kinaiweka Tanzania katika ramani ya Dunia na kuifanya kuwa nchi ya Kwanza kwa uzalishaji wa asali katika nchi za Afrika Mashariki na SADC; nchi ya Pili kwa uzalisahji wa asali barani Afrika; na nchi ya 14 Duniani kwa uzalisahji wa asali.
“Hii inaonyesha kuwa sekta ya ufugaji nyuki ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na ina nafasi kubwa ya kuendelea kukua na kuchangia zaidi katika Pato la Taifa na ajira kwa wananchi.”
Kuhusu usalama wa bidhaa hiyo ya asali pale inapopelekwa nchini china, Kitandula alisema Moja ya mkakati wao ni kuhakikisha asali inakuwa na ubora na ambapo wamefanya jitihada kubwa kuhakikisha asali hiyo ya Tanzania inakua na ubora kwa kuingia makubaliano na nchi nyingine duniani kutoka EU, UK soko la Marekani ili kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora wa kimataita kwa nchi zao.
“Tunamchakato ambao unafatilia uzalishaji wa asali yetu tangu shambani, inapoingia kiwandani, inapofungashwa na kusafirishwa, kote huku kuna viwango vya ubora ambavyo vimewekwa na kufatiliwa kuhakikisha kwamba asali inayotoka Tanzania inaendelea kuwa katika ubora unaotakiwa kimataifa”
“Hatua hizi zinalenga kuimarisha ushindani wa asali ya Tanzania katika masoko ya kimataifa na kuongeza Pato la Taifa kupitia mauzo ya nje ya bidhaa za nyuki. Mfumo huu pia unatoa uhakika kwa wateja wa kimataifa kuhusu usalama na ubora wa asali inayotoka Tanzania, hivyo kuongeza imani na upendeleo wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia.”
Kitandula alisema Kufunguka kwa soko la asali nchini China kunaenda pamoja na kutekeleza masharti kadhaa yaliyobainishwa kwenye Itifaki. Moja ya sharti ambalo wafanyabiashara wenye nia ya kuuza asali nchini China, nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani wanapaswa kutekeleza ni kuhakikisha kuwa Kampuni zao zinasajiliwa kwenye Mifumo ya Kimataifa ya Udhibiti wa Afya na Usalama wa Vyakula; Afya ya Mimiea; na Ulinzi wa Mazingira.
“Usajili wa Wafanyabiashara/Makampuni katika Mifumo hii hufanyika kwa njia ya kidigitali na Wizara yetu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeweka dawati maalum kwa ajili ya kusaidia Wafanyabiashara kujisajili. Hadi sasa ni Makampuni 12 tu ndiyo yamejisajili kwenye mifumo hii. Nitoe rai kwa Makampuni ambayo bado hayajasajiliwa yawasiliane na Wizara ili yaweze kusajiliwa.”
Sambamba na kufunguka kwa fursa hiyo, Kitandula alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafugaji nyuki na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki kwa kutoa Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT kwa vifaa na mashine mbalimbali zinazohusiana na ufugaji nyuki na kuongeza thamani mazao ya nyuki.
“Lengo la msamaha huu ni kuhakikisha kuwa tunaongeza kiwango cha uzalishaji na mauzo ya asali na mazao mengine ya nyuki nje ya nchi.”
Kitandula aliendelea kwa kumshukuru Rais samia suluhu hassan kwa kushiriki kwenye filamu mbili kubwa za kutangaza utalii kwani mafanikio makubwa yanayotokana na ushiriki wake yameonekana.
Kwa upande wake,Waziri wa Mamlaka ya forodha ya China, Yu Jianhua alisema makubaliano hayo yanaashiria hatua kubwa ya kufikia soko la Tanzania kwa wingi.
“Kwa mfano, tunaagiza asali zaidi ya tani milioni 32 kwa mwaka, ambayo ni takribani dola bilioni 60 za Kimarekani,” alisema.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best