November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania waonywa kujihusisha na dawa za kulevya

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Kilimanjaro

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa wito kwa watanzania kufanya kila linalowezekana kuachana na matumizi ya dawa za kulevya, huku kikionya wauzaji kuwa wanapanda mbegu ya uharibifu katika taifa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa (CCM), Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi,  katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kutembelea mikoa mitano.

Amesema kuna changamoto kubwa ya wananchi wengi kujikita kwenye matumizi ya dawa za kulevya ambazo zinaua msingi wa ufanyaji kazi kwa vijana.

Dkt.Nchimbi amesema vijana wengi kwa sasa wapo kwenye matibabu ya matumizi ya dawa za kulevya na wao hawafiki asilimia 10 ya wale walioathirika.

“Ninaomba wazazi na viongozi wa dini wote mshiriki katika kazi ya kuhakikisha tunafanya kila linalowezekana watoto wetu wanakuwa watoto bora na waandaliwe kuja kulitumikia taifa.

“Njia moja ya kuwaandaa ni kuwapa mazingira mazuri ya na kuwatenganisha na uwezekano wa kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya,”amesema.

Balozi Nchimbi ametaka kila mwenye uwezo ambaye anajihusisha na dawa za kulevya ajue anapanda mbegu ya uharibifu katika taifa lake.

Ametaka kila mtu apate moyo wa uzalendo wa kulipenda taifa lake na kuacha vitu vinavyoleta madhara ya muda mrefu kwa taifa.