December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakiwa kutenga muda wa mazoezi kuepuka magonjwa yasiyoambukiza

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

JAMII imetakiwa kujenga tabia ya kutenga muda wa ziada kwaajili ya kufanya mazoezi kwa lengo la kuimarisha afya na kupelekea kuepukana na magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza.

Kauli hiyo Juni 8,2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Gidlove Mbwaji wakati alipokuwa akihitimisha wiki ya Tamasha la Michezo na Vipaji liloshirikisha watumishi kutoka Hospitali hapo.

“Nitoe wito kwa jamii kwamba ni muhimu sana wafahamu mtaji mkubwa katika maisha yao ni afya yao, ni vizuri utumie muda unaopata kufanya mazoezi, na mazoezi yawe sehemu katika maisha yao” amesema Dkt.Mbwanji.

Aidha Dkt.Mbwanji amesema kuwa suala la afya ni muhimu hivyo ni vema kuzingatia suala la mazoezi ili kuweza kuimarisha afya zetu pamoja na kuepukana na magonjwa mbalimbali ambayo yanaweza kuwakumba.

Kwa upande wake Dkt.Uwesu Mchepange ni Mwenyekiti wa Kamati ya Tamasha la Michezo na Vipaji MZRH, amesema lengo la tamasha hilo kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ni kuwaleta watumishi pamoja na kuibua vipaji mbalimbali walivyonavyo.

“Tuliona tuwe na tamasha maalumu kwaajili ya watumishi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa lengo la kuwakutanisha waweze kuonyesha vipaji mbalimbali katika maeneo mbalimbali”amesema Mchepange

Kwa upande wao washiriki wa tamasha hilo la michezo na vipaji MZRH wameushukuru uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya chini ya Dkt.Godlove Mbwanji, kwa kuwa imekuwa sehemu ya burudani pamoja na kuwaimarisha kiafya na hivyo kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.

Tamasha hilo limefanyika kwa muda wa wiki moja chini ya udhamini wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya likihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta Kamba, maonyesho ya mavazi, maigizo, mpira wa pete, mpira wa wavu, ambapo washindi wamekabidhiwa zawadi ya pesa taslimu pamoja na vikombe.