Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online Muheza
MADIWANI na watendaji wa vijiji wametakiwa kusimamia kwa ukaribu zoezi la utambuzi wa kaya maskini ili kusiwepo na kaya hewa kuingizwa kwenye mpango wa wanufaika wa TASAF.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Halima Bulembo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kujenga uwelewa kuhusu sehemu ya pili ya awamu ya Tatu ya TASAF kwa madiwani na watendaji wa vijiji na kata wilayani humo.
Aliwataka kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu zoezi hilo ili kupata walengwa haswa na iwapo watabainia kuwaingiza walengwa ambao hawakidhi vigezo basi wawatoe mara moja.
Bulembo alisema lengo la serikali kuanzisha Tasaf ni kuwakwamua wananchi masikini wasiojiweza hivyo ni vyema watendaji wakawa wakali ili kusimamia kuwapata walengwa wanaohitajika.
“Wapo wazee wasiojiweza lakini wanakosa fursa unashangaa anaenda mtu ana wake watatu eti anataka Tasaf tuwe wakali kwenye hili tusimamie ili tuweze kuwapa serikali fursa ya kufikia malengo yao,”amesisitiza Bulembo.
Aliongeza kuwa, “madiwani na viongozi wa vijiji nyie ndio mnaishi na watu katika maeneo yenu, hivyo nisingependa kuona hili zoezi linaharibiwa kwa kuingizwa walengwa wasiostahili kwa ajili ya kunufaika na kuwaacha wanaostahili wakiendelea kupata tabu,”amesema DC Bulembo.
Hata hivyo mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAF, Kelvin Simon amesema kuwa mpango huo umechangia kupunguza umaskini wa mahitaji ya msingi hadi kufikia asilimia 10 huku umaskini uliokidhiri umeweza kupungua kwa asilimia 12.
“Kwa awamu hii ya Tatu mpango unatarajiwa kufika maeneo yote ya Tanzania bara na visiwani kwa kuzitambua kaya zote na kuweza kushiriki katika kusaidiwa kiuchumi,”amesema.
Madiwani walioshiriki kikao hicho wameipongeza serikali kwa kuja tena na mpango huo huku wakiahidi kuhakikisha wanasimamia ipasavyo kuwapata walengwa husika.
“Malalamiko yamekuwa mengi sana kwenye maeneo yetu kwamba mpango huu wanaonufaika ni watu wenye maisha yao hivi sasa tunakwenda kuwa wakali kwenye hili hatutavumilia kuona hali hii ikiendelea katika awamu hii, “walisisitiza.
More Stories
Wafanyabiashara wakutana Dar,kujadili hali ya biashara
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo