Na Irene Clemence, TimesMajira Online
JUMLA ya Watahiniwa 1,397,370 wa Darasa la saba kati yao wavulana wakiwa 654,652 sawa na asilimia 46.85 na wasichana 742,718 sawa na asilimia 53.15 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa siku mbili kuanzia kesho Septemba 13.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam mapema Leo hii Katibu Mtendaji wa Baraza la Mtihani Tanzania(NECTA) Dkt Said Ally Mohammed
amesema mtihani huo wa darasa la saba utafanyika katika shule za msingi 18,320 kwa Tanzania Bara .
Dkt Mohammed amesema kati ya watahiniwa 1,397,370 waliosajiliwa kufanya mtihani mwaka 2023 watahiniwa 1,334,269 watafanya mtihani kwa lugha ya kiswahili na watahiniwa 63,101 watafanya mtihani kwa lugha ya kingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia.
Amesema watahiniwa wenye Mahitaji maalumu waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 4,583 kati yao 101 ni wasioona 1,321 wenye uoni hafifu 1,125 wenye uziwi, 549 ni wenye ulemavu wa akili na akili na 1,487 wenye ulemavu wa viungo.
“Katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi jumla ya masomo sita yatatahiniwa ambayo ni kiswahili, kingereza, sayansi na teknolojia, hesabu, maarifa ya jamii na stadi za kazi pamoja na uraia na maadili”amesema Dkt Mohammed
Aliongeza kuwa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwa kuwa hupima maarifa na umahiri wa wanafunzi katika masomo waliyosoma katika elimu ya msingi.
Alisisitiza kuwa matokeo ya mtihani huo hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya Sekondari hivyo ni muhimu kwa wanafunzi, wazazi na jamii nzima kwa ujumla katika taifa .
Akizungumza kuhusu maandalizi Dkt Mohammed amesema yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani pamoja na nyqraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika halmashauri na Manispaa zote nchini.
“Maandalizi yote kwa ujumla kwa ajili ya watahiniwa yamekamilika ikiwemo wenye Mahitaji maalumu kamati za mitihani za mkoa na Halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu”amesema
Aidha alitoa wito kwa kamati za mitihani za mkoa na Halmashauri kuhakikisha kuwa usalama wa vituo vyote vya mitihani unaimarishwa na kwamba vituo hivyo vinatumika kwa kizingatia mwongozo uliotolewa na baraza la mitihani la Tanzania.
Kwa upande wa wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia mtihani huo amewataka kufanya kazi yao kwa umakimi na uandilifu wa hali ya juu .
“Wasimamizi wanapaswa kuhakikisha wanafanya kazi ya usimamimizi wa mtihani huu kwa weledi na kwa kizingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mtahiniwa apate haki yake”alisema
Katibu mtendaji huyo amesema kwa upande wa watahiniwa wenye Mahitaji maalumu waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine .
Katika hatua nyingine Dkt Mohammed aliwataka wamiliki wa shule kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mtihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mtihani katika kipindi chote Cha kufanyikaji wa mtihani huo.
“Baraza halitosita kukifutia kituo chochote Cha mitihani endalo litajiridhisha pasipo shaka kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mitihani ya taifa “alisisitiza Dkt Mohammed
More Stories
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa