Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
JUMLA ya watahimiwa 566,840 Wanatarajia kuanza kufanya mtihani wa kidato cha nne kesho Novemba 14 hadi Disemba 1 ambapo kati yao watahiniwa wa shule ni 535,001 na watahiniwa wa kujitegemea ni 31,839.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, Novemba 13, 2022, Kaimu katibu Mtendaji wa Baraza la mitihani Tanzania (NACTE) Athumani Amasi amesema mtihani huo wa kidato cha nne utafanyika katika jumla ya shule za sekondari 5,212 pamoja na vituo vya kujitegemea 1,794.
Amesema watahiniwa wa shule 535,001 waliosajiliwa ambapi wavulana ni 247,131 sawa na asilimia 46.19 na wasichana 287,870 sawa na asilimia 53.81
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea 31,839 waliosajiliwa wavulana ni 13,556 sawa na asilimia 42.58 na wasichana ni 18,283 sawa na asilimia 57.42 huku watahiniwa wenye mahitaji Maalumu wakiwa 13 ambapo wenye mahitaji uoni hatifu ni 2 na wasioona ni 11.
” Mwaka 2021 idadi ya watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 538,024 hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 28,816 sawa na asilimia 5.36 kwa mwaka 2022 ukilinganisha na mwaka 2021″amesema Amasi.
Vilevile amesema kwa upande watahiniwa wenye mahitaji maalumu 852 na kati yao 480 ni wenye uoni hafifu, 62 ni wasioona, 19 wenye ulemavu wa kusikia, na 152 ni wenye mtindio wa akili na 139 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.
Aliongeza kuwa watahiniwa 12,090 wamesajiliwa kufanya mitihani wa maarifa ( QT) ambapo wanaume ni 4,096 sawa na asilimia 33.88 na wanawake ni 7,994 sawa na asilimia 66.12 huku wenye mahitaji maalumu wakiwa 36 ambao ni wenye uoni hafifu.
Kwa upande wa maandalizi Amasi alisema yamekamilika ikiwa ni pamoja kusambazwa kwa mtihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote maalumu zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar.
Aidha alitoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri, Manispaa, Jiji pamoja na Miji kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya kitaifa zinazingatiwa.
“Baraza linatoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kufanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu ambapo wasimamizi wanaelekezwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa”alisisitiza.
Hata hivyo Kaimu katibu huyo aliwataka wasimamizi, wamiliki wa shule, walimu na wazazi na walezi kutojiusisha au kushiriki kwa namna yoyote na vitendo vya udanganyifu wa mitihani.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa