December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watafiti wabuni bidhaa kutumia maganda ya matunda

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online

KUTOKANA na Dunia kuelekea kwenye matumizi ya nishati mbadala ili kutunza na kuokoa mazingira ,watafiti wakiwemo wanaotoka nchini Tanzania wameendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kupata nishati safi na rahisi kwa wananchi.

Kutokana na hali hiyo watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar esalaam ,wamefanya utafiti wa maganda ya papai nanasi ,embe na tikiti maji na kupata bidhaa tofauti ambazo zinaweza kutumika kama mafuta ya taa,vitakasa mikono,nishati mbadala ya mafuta ya kwenye magari,spiriti na matumizi ya kwenye maabara kwa ajili ya kufundishia wanafunzi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ,Mtafiti kutoka chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt.Jovin Emmanuel amesema bidhaa hizo zinaenda sambamba na utunzaji wa mazingira kwani kinachotumika ni takataka ambazo huwa zinatupwa.

“Kwa hiyo hapa utaona faida ni nyingi tena kubwa ,maana kama unavyojua maganda ni takataka ambazo huwa zinatupwa halafu zinaoza na kusababisha vimelea vya magonjwa,  sasa sisi tunazichukua na kutengeneza bidhaa ambazo ni muhimu kwa matumizi ya binadamu ambazo zinakuwa katika viwango tofauti.”amwsema Dkt.Emmanuel

Amesema bidhaa hiyo ipo tayari kwa matumizi kwa sababu imeshafanyiwa utafiti isipokuwa changamoto iliyopo ni mtaji wa kitengeneza bidhaa hiyo kwa wingi.

Amwtumia nafasi hiyo kuwasihi wadau na yaasisi mbalimbali kikiwemo chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kufadhili mradi huo ili bidhaa hizo ziweze kuzalishwa kwa wingi na tafiti hiyo ilete matokeo chanya yaliyokusudiwa kwa bidhaa kufika hadi kwa wananchi kwa ajili ya matumizi.

Hata hivyo amesema kwa sasa kama kuna mtu anahita moja ya bidhaa hizo anatengezewa kwa oda maalum.

Dkt.Emmanuel amesema wanayatumia maonesho hayo kutangaza bidhaa hizo huku akiwaasa wadau mbalimbali kupita kwenye banda lao kujionea bidhaa hizo.