Na Penina Malundo, timesmajira, Online
Mkurugenzi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu,Rashid Mafutaa ametoa wito kwa watoa huduma za afya kushirikiana na wadau wa mashirika yanayotoa huduma kwa watu wenye ulemavu nchini kuimarisha huduma za utambuzi wa mapema kwa watoto wenye ulemavu katika jamii na vituo vya afya.
Mafutaa ameyasema hayo mapema wiki hii alipokuwa akifungua kikao kazi cha kutengeneza mpango mkakati wa taifa wa utengemao (National Rehabilitation Strategic Plan-NRSP) jijini Dodoma.
“Mhe. Rais alisisitiza katika kikao chake na watu wenye ulemavu kuimarisha suala la utambuzi wa mapema kwa watoto wenye ulemavu katika jamii vilevile katika vituo vya kutolea huduma za afya” amesema Bw. Mafutaa na kuwataka wataalam kutengeneza Muongozo ambao utaenda kutusaidia katika uimarishaji wa masuala ya utambuzi wa mapema kwa watoto wenye ulemavu katika jamii
Mkurugenzi huyo ameendelea kusisitiza kuwa endapo Jamii itawahi mapema kumgundua mtoto mwenye tatizo la ulemavu itasadia pia katika kuwahi kumuweka kwenye matibabu na kupunguza athari ya kiungo kilichopata changamoto hiyo na kurejea katika hali yake ya kawaida na kumfanya muhusika kujimudu na kuendelea na shughuli zake za kila siku kama kawaida.
“Mfano kama mtu ana changamoto ya usikivu naamini ukimuwahi mapema kumgundua na akapata huduma za mapema atakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kupata usikivu wa awali na kurudi katika hali yake ya kawaida na kuendelea na shughuli zake” amesema Mafutaa
Aidha, Mkurugenzi Mafutaa amewataka wadau kuungana pamoja katika kuunga mkono jitihada mbambali za serikali za utambuzi wa mapema kwa watoto wenye ulemavu na kuelekeza nguvu ya pamoja katika kutengeneza mpango mkakati wa utengemao ambao utasaidia kufanya utetezi kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum sambamba na kuchochea kuboresha sera na kutekeleza huduma zinazohusu utengemao.
“Tunawashukuru Shirika la Blind Mission(CBM) kwa kufadhili mkutano huu muhimu kama wadau kwa watu wenye ulemavu nchini”.
Aidha, kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika yanayotoa huduma za watu wenye ulemavu nchini,Elirehema Kaaya ameshukuru Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuandaa Mpango Mkakati wa Taifa wa utengemao ambao ni wa kwanza kuwepo nchini pamoja na kuwashukuru wadau wote wa mtandao huo kwa kuwa pamoja katika ushiriki wa mkutano huo muhimu.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba