January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa taasisi za umma mara baada ya kumaliza ziara yao ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere.

Wataalamu wa ndani JNHP2115 wapongezwa

Na James Mwanamyoto, Rufiji

VIONGOZI wakuu wa Kitaifa wastaafu wakiwemo Marais na Mawaziri Wakuu wamewapongeza wataalamu wa ndani kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Haydropower Project) ambao ujenzi wake umefikia asilimia 54.

Pongezi hizo wamezitoa walipoutembelea mradi huo kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi na kutoa ushauri utakaoboresha ukamilishaji wa ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kitaifa unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alisema amefurahishwa na namna wataalamu wa Kitanzania walivyoweza kusimamia mradi huo kwa ustadi mkubwa hivyo amewapongeza kwa kutumia vema taaluma yao kusimamia ujenzi wa mradi huo wa kufua umeme kwa nguvu za Maji wa Julius Nyerere.

Naye, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete aliwapongeza waliohusika kuchora mchoro wa mradi, wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa mradi huo na kwa kipekee alimshukuru Rais wa Awamu ya Sita Samia Suluhu Hassan kwa kuupokea mradi na kuuendeleza.

Aidha, Dkt.Kikwete alimpongeza Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kwa uamuzi wake wa kutafuta fedha na kuanza ujenzi wa mradi huo ili kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Dkt.Kikwete amesema, ndoto ya Baba wa Taifa ilikuwa ni kujenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme, lenye shughuli ya utalii, litakalopunguza mafuriko sehemu ya chini ya mto Rufiji na kuwezesha kilimo cha umwagiliaji kitakacholisha takribani watu milioni ishirini, hivyo ametoa wito kwa wadau wa kilimo waanze kujipanga kutumia fursa ya kilimo cha umwagiliaji.

Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela amesema, watanzania wanapaswa kujivuna kwa kutekeleza mradi huo kwa fedha zao wenyewe na kuongeza kuwa, watanzania wajisikie fahari kwani mradi huo unasimamiwa na wazawa ambao wameonesha uzalendo kwa taifa kwa kusimamia vema ujenzi wake.

Malecela amefafanua kuwa, tangu taifa lipate uhuru halijawahi kutekeleza mradi mkubwa kama huo wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere hivyo watanzania hawanabudi kujivunia mradi huo.

Akizungumzia ujenzi wa mradi huo, Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya alimpongeza Waziri wa Nishati, Medard Kalemani na wataalamu wake wa kitanzania kwa kujitoa na kuwajibika kikamilifu katika usimamizi wa ujenzi wa mradi huo.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda aliipongeza Wizara ya Nishati kwa usimamizi mzuri wa mradi huo mkubwa ambao ujenzi wake umefikia asilimia 54 na kutoa wito kwa watanzania kuhakikisha mradi huo unatumika vizuri ili kukamilisha ndoto ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Waziri wa Nishati,Medard Kalemani alisema, mradi ukikamilika nchi itakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye gharama nafuu hivyo ametoa wito kwa wenye nia ya kuwekeza kujitokeza na kuwekeza kwenye shughuli za kilimo, umwagiliaji na utalii.

Dkt.Kalemani alisisitiza kuwa, kupitia uzoefu wa usimamizi wa mradi huo watanzania tumejifunza kwamba hata miradi mingine itakayoanza kutekelezwa itasimamiwa na watanzania wenyewe kwani wataalamu wazawa wanao uwezo huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mohamed Mchengerwa aliwataka viongozi wote wanaosimamia miradi ya mikubwa ya kimkakati na mingine kuhakikisha ina kamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Mchengerwa alifafanua kuwa, Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan amedhamiria kukamilisha mradi huo ifikapo mwakani ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi mingine ya kimkakati na kutoa wito kwa wasimamizi wa miradi kusimamia vizuri kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotumika na kuwaonya watakaokwamisha miradi kuwa watachukuliwa hatua stahiki.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa aliwahakikishia watanzania kuwa, miradi yote mikubwa ya kimkakati itakamilika kwa wakati kama ambavyo Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan amedhamiria.

Ujenzi wa Mradi huo wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Haydropower Project) unatarajia kukamilika tarehe 14 Juni, 2022 na utakuwa na uwezo wa kufua umeme wa Megawati 2115.